WAZIRI NDEJEMBI AUNDA KAMATI KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI MWANZA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Kamishna wa Ardhi nchini Bwana Mathew Mhonge kuunda kamati mara moja kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa ardhi kwa kiwanja namba 01, Kitalu R kilichopo mtaa wa barabara ya Nyerere .
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo leo Februari 10, 2025 akiwa kiwanjani hapo jijini Mwanza alipofanya ziara mahususi kwa ajili ya kushuhudia na kusikiliza pande mbili za malalamiko baina na mmiliki Z.E.K Ladhan Ltd na Halmashauri ya jiji la Mwanza.
Waziri huyo ameagiza hadi kufikia ijumaa ya wiki hii (februari 14) kamati hiyo iwe tayari imepatikana ikihusisha wajumbe kutoka Wizara yake na Mkoa wa Mwanza aidha ifanye kazi ya kupitia nyaraka kwa siku saba kuanzia februari 17, 2025 na itoe mapendekezo ya nani mmiliki halali na nini kifanyike.
Sambamba na hilo ametoa wito kwa jamii kuendelea kufuata sheria wakati wanapotaka kumiliki ardhi ili kujiepusha na migogoro na kwa upande wa watumishi wa serikali (Sekta ya Ardhi) amewasihi kuendelea kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi wao kwa mujibu wa kanuni na sheria.
Akijibu hoja ya mwananchi mmoja aliyetaka kufahamu hatma ya wananchi waliovamia eneo la Mamlaka ya Viwanja vya ndege katika Manispaa ya Ilemela na kuzuiwa kuviendeleza, Mhe. Ndejembi amesema serikali inashughulikia suala hilo na siku za usoni itaketi nao kuzungumza na kumaliza mgogoro huo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru Waziri wa Ardhi kwa utendaji wake unaolenga kumaliza migogoro ya ardhi nchini hususani mkoani humo na amemuahidi kushiriki vema kwenye uundaji wa kamati hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.