Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (MB) mapema leo ijumaa tarehe 23 Januari, 2026 ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa kituo cha kuratibu ufuatiliaji na uokozi katika ukanda wa ziwa Victoria wilayani Ilemela.

Akiongea na wananchi baada ya ukaguzi huo Dkt. Nchemba amesema Serikali ya awamu ya sita inajali maisha ya wananchi wake na kwamba inajipambanua kwa dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kutekeleza miradi mikubwa hata iliyoshindikana siku za nyuma.

“Jambo hili linahusisha masuala ya kidharula, watendaji kwenye mradi huu msisinzie hata kidogo maana mtaleta maafa kwa kuangamiza maisha ya watu na vifaa vya kisasa vilivyowekwa kwa gharama kubwa kwa fedha ambazo Mhe. Rais ameweka hapa pamoja washirika wenzetu” Mhe. Waziri Mkuu.

Akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu, Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof Makame Mbarawa amesema ukanda wa ziwa victoria umekua na changamoto kubwa ya ajali za majini ambapo takribani watu 20 wamefariki maji na ndipo Serikali ikaamua kuwa na kituo hicho kwa ajili ya uokozi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) Mohamed Salum amesema Kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kimataifa wa Afrika Mashariki wa kuzuia matukio ya ajali na upotevu wa maisha ya watu ambao uliidhinishwa na Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki mwaka 2007.

Aidha, amebainisha kuwa mnamo mwaka 2022 hadi 2025 mradi huo ulianza rasmi kutekelezwa kwa pamoja na Mataifa ya Tanzania na Uganda ambapo umelenga kuimarisha usalama wa vyombo kwa kuongeza wigo wa ufuatiliaji wa ajali kwenye vyombo vya usafiri pamoja na wavuvi katika eneo la maziwa.

Aidha, amebainisha kuwa kituo hicho rasmi cha utafutaji na uokoaji na kupata taarifa halisi za hali ya hewa kwa gharama za Tshs. Bilioni 19.8 kwa upande wa Tanzania huku ikijumuisha gharama za vituo vya Uokoaji vitatu, Boti, Maboya pamoja na jengo katika eneo la kituo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.