CCM YAIPONGEZA SERIKALI UJENZI WA BARABARA YA LAMI BUHONGWA- IGOMA.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza leo 27, Mei 2024 imekagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Lami yenye urefu wa Kilomita 14 (Buhongwa - Kishiri- Igoma)Jijini Mwanza na kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa Usimamizi wa mradi huo na imemtaka kuendelea kusimamia vema mradi huo.
Akiongoza Kamati hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Mhe. Michael Lushinge amemtaka Mkandarasi Zhongmei Engineering group Ltd anayejenga barabara hiyo kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 22.7 kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kwa mujibu wa mkataba ili wananchi wa Kata nne zinazopitiwa na mradi wanufaike.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema chini ya usimamizi wake kupitia Idara ya ujenzi Jiji la Mwanza pamoja na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) atahakikisha ujenzi unakwenda kwa kasi ili hadi kufikia Februari 2025 uwe umekalimika na kuwandolea wananchi adha ya usafiri.
Ameahidi kuketi na TARURA, MWAUWASA na TANESCO ili kuhamisha kwa hataka miundombinu na kuweza kuharakisha mradi na kwamba atazungumza na ofisi husika ili wakandarasi wapate fedha kwa wakati na kuweza kutekeleza mradi huo wenye manufaa makubwa kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Erick Mvati amesema kuwa mradi huo wa kuboresha miundombinu ya barabara utahusisha ujenzi wa barabara pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Mshauri kwenye Makao Makuu ya Jiji, uwekaji wa taa 470, Makaravati na Mitaro kwa mkataba wa kuanzia Septemba 2023 na hadi Februari 2025.
Ameongeza kwamba Mkandarasi hadi sasa ameshalipwa Shilingi Bilioni 3 na ameomba kuongezewa Milioni 600 na kwamba changamoto kubwa inayoukabili mradi huo ni gharama za uhamishaji wa miundombinu ya Maji, Simu na Umeme pamoja na nyumba zilizopo kwenye eneo la mradi lakini zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.