Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Bi. Mariam Msengi amewataka viongozi na watendaji wa chama cha ushirika Nyanza kuwasimamia wakulima wa zao la pamaba ili wapate pembejeo kwa wakati, haraka na kwa urahisi kama yalivyo malengo ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Bi. Msengi ametoa wito huo leo Januari 30, 2026 wakati akifungua mkutano wa 34 wa chama kikuu cha ushirika cha Nyanza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda katika ukumbi wa Bomani.

Ameendelea kwa kuwasisitiza viongozi kuwa wawazi kwa wanachama kwa kutumia mifumo ya kidigitali katika upimaji na uuzaji wa zao la pamba kama jinsi ambavyo serikali inaelekeza.

"Niwasihi viongozi wa vyama vya ushirika kuhakikisha vipimo vya kidigitali vinatumika ipasavyo sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kunufaika kikamilifu na mifumo hiyo." Amesema Bi. Msengi.

Aidha, ameongeza kuwa serikali inaendelea kusimamia kwa karibu mfumo wa stakabadhi za ghala katika uuzaji wa mazao ya mikunde kama choroko na dengu ili kuhakikisha kunakua na uimara wa ubora wa mazao pamoja na ushindani wa bei katika masoko.

Naye, Mrajisi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza Bi. Hilda Boniface amewataka wakulima wa pamba kuandaa mazao kwani chama cha Nyanza kinakwenda kufungua kiwanda cha kuchakata zao hilo katika halamashauri ya Wilaya ya Magu.

Sambamba na hilo amewataka wananchama kuchangia katika mambo amabyo yanaweza kujenga na kuleta maendeleo katika chama ikiwa ni sambamba na kutoa michango kwa wakati na kutatua migogoro yote inayotokana na vyama vya kimsingi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.