Jumla ya wanawake 50,000 hapa nchini kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hupata maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi na hivyo kusababisha asilimia 37 ya wanawake wanaogundulika na ugonjwa kufariki kila mwaka.
Hayo yamesemwa jijini hapa na Afisa Mpango wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na watoto Pricella Kinyunyi alipokuwa akieleza lengo mahususi la serikali kuanzisha chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri kuanzia miaka 9- 14 kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya afya kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.
Alisema wagonjwa wengi wa saratani ya mlango wa kizazi hawapati mapema huduma za ugunduzi na matibabu sahihi kwa wakati hali inayosababisha vifo.
“Takwimu kutoka hosipitali ya ocean Road inaonyesha kwamba, saratani ya mlango wa Kizazi inachangia kwa asimilia 36 ya saratani zote na asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi wanajitokeza katika hatua ambayo tayari saratani imesha sambaa maeneo mengine mwilini,” alisema.
Aliongeza kuwa chanjo hiyo ya saratani ya mlango wa kizazi ni salama na imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani na kwamba majaribio ya matumizi ya chanzo kwa mara ya kwanza yalianzia mkoani Kilimanjaro mwaka 2014 na haikuwa na madhara ya kiafya.
“Matokeo ya chanjo hiyo yalikuwa ni mazuri mkoa ulifikia asilimia 90 ya uchanjaji, lengo hasa lilikuwa ni kupata uzoefu wa kujifunza kwa vitendo kabla ya kwenda nchi nzima,” aliongeza.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela katika kuhakikisha ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi unatokomezwa, amewataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji na wenyeviti wa halmashauri kuhakikisha wanahamasisha vijana wengi kwenye maeneo yao ili waweze kupata chanjo hiyo.
“ Hatuwezi tu kuruhusu watu kupata huduma za tiba peke yake, lazima tuhakikishe program za chanjo katika mkoa wetu zinaimarishwa,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa za serikali, mkoa wa Mwanza umetekeleza zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi ambayo ilizinduliwa rasmi April 23 mwaka jana, na kuandikisha jumla ya mabinti 31,291 wenye umri chini ya miaka 14, ambapo uliweza kuchanja jumla ya mabinti 24,628 ikiwa ni sawa na asilimia 79 ya ufanisi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.