FUNGUENI BENKI YENU YA USHIRIKA MAPEMA MUONGEZE MAPATO: RC MAKALLA
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija ameishauri Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuharakisha uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ili kuwa na chombo imara cha kiuchumi.
Akizungumza Jumatatu hii kwenye viwanja vya Furahisha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati wa ufunguzi wa wiki ya Vyama vya Ushirika wa akiba na mikopo,amesema hakuna sababu ya kuchelewa kuwa na Benki wakati uwezo wa kuwa na Taasisi hiyo wanao.
"Kisheria kuwa na Benki lazima uwe na mtaji wa Sh Bilioni 15 lakini najua sasa mmekaribia kufikia kiwango hicho, fanyeni juu chini mfikie malengo hayo ili mjenge chombo imara cha kiuchumi hapa nchini." Ludigija.
Amesema amesikia taarifa ya baadhi ya Saccoss zimekopesha zaidi ya Shs bilioni 100 na nyingine trioni moja ambayo ni ni hatua kubwa sana ya kimaendeleo.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Mwanza, kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Ndg.Daniel Machunda amesema wana jumla ya Saccoss 371 na wanachama 14,638 huku wakiwa na mtaji wa Shs bilioni 12.7.
"Ndugu mgeni rasmi vyama vyetu vya Ushirika wa akiba na mikopo vimekuwa msingi imara wa kuinua vipato vya wananachama wake ambapo kila mwaka mikopo ya Shs bilioni 12.5 hutolewa". Machunda.
Kuhusu maendeleo ya vyama vya Ushirika wa akiba na mikopo nchini, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Dkt. Benson Ndiege amesema sasa wanataka kutoa wigo zaidi kwa kila mwanachana kuwa na uwezo wa kujiunga na Saccoss nyingi tofauti na sasa kuwa moja pekee.
"Nimetembelea baadhi ya nchi hapa Afrika na Ulaya wenzetu wamepiga hatua zaidi na kuwa na wanachama wengi kutokana na namna walivyoziboresha,ni wajibu wetu kufanya mageuzi hayo",Dkt.Benson
Kilele cha wiki ya Vyama vya Ushirika wa akiba na mikopo ni Oktoba 26 mwaka huu ambapo Tanzania inajumuika na Mataifa mengine ulimwenguni kusheherekea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.