Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Magufuli amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo pamoja ukarabati wa meli za MV. Victoria na MV. Butiama kuhakikisha zinakamilika kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi.
Pia amemuagiza Msimamizi wa Mamlaka ya Bandari Mwanza Kusini, Moris Mchindiyuza kuangalia maslahi ya vibarua wanaopakia na kupakua mizigo kwenye bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kusajili majina yao ili waunde chama chao.
Rais Dkt. Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli mbili za MV.Victoria na MV. Butiama katika eneo la Bandari ya Mwanza Kusini.
“Wahandisi na Wizara ya Uchukuzi hakikisheni kazi hii inafanyika, haiwezekani serikali ikatoa zaidi ya sh. bilioni 152 kujenga meli na kukarabati nyingine halafu mradi uchelewe.Msichelewe hata siku moja, hiki kitendo cha mkandarasi kutopeleka documents (nyaraka) kisirudiwe tena, hata wizara haziwasiliani,”alisema
Amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha za Watanzania hivyo na kushangaa mkontena 56 ya mradi wa meli mpya kukwama bandarini,
“Meneja, contractor (mkandarasi), simamieni kazi vizuri na hakikisheni meli zinaingia majini kwa muda uliopangwa.Lazima niwaeleze ukweli , mkandarasi yuko hapa kwa sheria namba 17 ya 2017. ”
“Najua kuna mchezo wa kuuza vifaa , mliuza Crane hakikisheni mnazirudisha, mwambieni Kakoo (Deusdedit), hayafahamu yaliyofanyika hapa.Mimi nayafahamu.”
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya ukarabati wa meli za MV. Victoria na MV. Butiama, msimamizi wa mradi huo Meja Abel Gwanafyo alisema kazi hiyo ilianza Machi 5 mwaka huu ambapo wameanza kuondoa injini zote za zamani makangavuke matano (jenereta), na vifaa vya hydroric.
Amesema meli hizo zimepandishwa kwenye chelezo na kuzifanyia ukaguzi kuona kama maji yana uhusiano wa chuma hivyo kazi ya kufunga injini mpya itafanyika baada ya kuwasili Machi mwakani ambapo injini hizo zitawasili nchini Septemba mwaka huu.
Naye Meja Mapunda ambaye ni msimamizi wa mradi wa meli mpya amesema usanifu umekamilika na kuhakikiwa huku ukataji wa vyuma ukiwa kwenye asilimia 30 ambapo meli hiyo itakuwa na injini mbili za kuiendesha huku ujenzi ukitarajiwa kuanza Machi mwakani.
Alisema baada ya kukamilika kwa meli hiyo itafanyiwa jaribio la uzani kabla ya kuanza safari ambapo kazi inayofanyika sasa ni kusafisha eneo la kujengwa kwa chelezo cha tani 4000 kitakachotumika kwa ujenzi wa meli hiyo itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 200 za mizigo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport (SMT) Major Songoro alisema wanakarabati meli za MV. Butiama na Mv. Victoria kwa kushirikiana na kampuni ya KMT. Co. LTD ya Korea alisema watajitahidi kukamilisha kazi kwa wakati.
“Tunashukuru kwa maelekezo ya Rais Magufuli na sisi kama wakandarasi wazawa (Watanzania), kazi hii tutaifanya na kuikamilisha kwa wakati kutokana na ujuzi, uwezo tuliuonao tukiongeza na wa wenzetu KMT.Co. utatusaidia kusonga mbele zaidi,” alisema Songoro.
Aidha, Rais Magufuli alimuagiza Msimamizi wa Bandari (TPA) ya Mwanza Kusini kuangalia maslahi ya makuli wanaobeba mizigo kwenye bandari hiyo kulingana na mizigo wanayobeba kwani wakizeeka hawatakuwa na uwezo huo tena.
“Meneja wa hapa yuko wapi? Hebu njoo ueleze mipango ya maslahi ya hawa wafanyakazi, maana mikono na viuno vinauma.Wanalipwaje na vifaa hawapewi,”alisema Mhe.Rais.
Msimamizi huyo wa bandari (Mchindiyuza) alisema wao ni wasimamizi tu isipokuwa vibarua hao wanalipwa kwa mikataba waliyoingia na kampuni zinazotoa huduma kwenye bandari hiyo.
Kutokana na maelezo hayo Mhe. Rais Dkt. Magufuli amemuagiza meneja huyo kuangalia maslahi ya vibarua hao na kuorodhesha majina yao waunde chama chao, na meli mpya itakapoanza kufanya kazi atakuwa mdhamini wao na kuonya yasiongezwe majina mengine kwa udugu wa meneja huyo.
Kabla ya kutoa maagizo hayo Mhe. Rais Magufuli alimpa nafasi mmoja wa makuli wa bandari hiyo Kassim Rashid ambaye alidai wanafanya kazi kubwa na kulipwa fedha kidogo.
“Nimefanya kazi hapa kwa miaka 10, Mheshimiwa Rais yanayofanyika hapa yanatuumiza, watumishi wa bandari wanalipwa fedha nyingi na wafanyabiashara, sisi tunalipwa kidogo na hatupewi vifaa vya kujikinga,”alisema Rashid huku akihofia kufukuzwa kazi.
“Wala hakuna wa kukufukuza.Huyu msifukuze, ukimfukuza na wewe na kufukuza.Ila na wewe (Rashid) usiache kufanya kazi.Meli hizi zimeharibika na nyingine inajengwa.Huyu mkuu wa TPA atachukua majina yenu na meli ikianza kazi mimi nitakuwa mdhamini wenu.Hamuwezi kunyang’anyana ng’ombe kabla hajazaa,”alisema Rais Magufuli.
Alimuonya Mchindiyuza kuwa wasiongezeke wengine wa kuletwa hapo kwa sababu ya undugu na kufahamiana na vibarua waliopo baada ya kuorodheshwa wapewe vitambulisho ili mwishowe wasizuiwe kuingia bandarini hapo kufanya kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.