HAKUTAKUWA NA NYONGEZA HATA SIKU MOJA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI WA TACTIC - WAZIRI MCHENGERWA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 14.7, katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko la Kirumba na barabara ya kuzunguka soko yenye urefu wa kilomita 2.9, huku ikitarajia pia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 7.3 katika ujenzi wa soko la samaki Mkuyuni na kuwataka Wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba.
Waziri huyo wa TAMISEMI ameyasema hayo mapema leo Oktoba 16, 2024 alipokuwa akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa soko la kirumba na barabara ya kirumba katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na Soko la Samaki Mkuyuni katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia miradi ya uboreshaji Miji Tanzania (TACTIC).
Aidha Akishuhudia utiaji saini mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo, Waziri Mchengerwa, ameziagiza Halmashauri husika kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi usimamizi na utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na wananchi wa Mwanza na maeneo mengine kote nchini wanufaike na uwekezaji huo ambao Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuufanya.
"Rais wetu amekusudia kwenda kuleta mapinduzi makubwa ya kuboresha Miji, kuboresha Majiji, na Manispaa, miradi hii sio kwa bahati mbaya, miradi hii sio starehe, miradi hii ni mafanikio makubwa ambayo wananchi wa Mwanza mnakwenda kuyapata kupitia miradi hii".
Kadhalika Waziri huyo amesema miradi hiyo inakwenda kuwagusa Watanzania wote kwa wenye kipato na wasio na kipato, wapo watakaokwenda kunufaika na fedha za miradi hiyo na wapo watakaonufaika kutumia sehemu ya miradi hiyo kama barabara, na kama walikuwa wakipata adha ya kutembea kwa nusu saa sasa watatumia dakika tano kwa barabara za lami zitakazokwenda kujengwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameishukuru Wizara ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kuruhusu mikataba ya namna hiyo kuwekwa hadharani na kwa namna ambavyo wamekuwa wakiwashirikisha wananchi hatua kwa hatua kuelekea ukamilishaji wa utiaji wa saini wa mikataba hiyo.
Miradi ya ujenzi soko la Kirumba, barabara ya soko pamoja na soko la samaki Mkuyuni, itatekelezwa kwa miezi 12 kuanzia Novemba mosi mwaka huu hadi Oktoba 31 mwakani, Aidha miradi hiyo ya Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC), inayofadhiliwa na serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia, wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 410, inayanufaisha majiji 5, Manispaa 16 na Miji 24 kote nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.