Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amewapa siku 90 Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuhakikisha wanapeleka Michango ya watumishi ya zaidi ya Tshs Bilioni 2 kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa mujibu wa sheria ili kuepusha Migogoro.
Mhe Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo mapema leo jumatatu wakati wa Mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani lililokutana kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kubaini kuwa mwaka 2015/16 Halmashauri hiyo haikuwasilisha michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii pamoja na wanachama kukatwa fedha.
"Huo ni uzembe mkubwa na ndipo changamoto ilipo, hata kama jambo hilo limekwama Hazina lakini mmepeleka barua zamani sana yaani tangia mwaka 2015 hamjafuatilia kwenye ofisi husika kujua tatizo liko wapi ili kufuta hoja, na kote nilikopita hapa ndio nasikia kuna hoja ya namna hii." Mkuu wa Mkoa.
Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani amefafanua kuwa asili ya hoja hiyo ni kuwa Halmashauri ilikua inalipa mishahara yenyewe na ilikua inawakata fedha watumishi kwa ajili ya michango hiyo lakini haikuwasilisha kwenye mifuko husika.
Hata hovyo, ndugu Waziri amesema Mwaka 2020/21 Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ilifanyiwa ukaguzi na kupata Hati Inayoridhisha na kwamba kuanzia 2013/14 hadi 2020/21 Halmashauri hiyo imekua na jumla ya hoja 30 ambazo hazijatekelezwa kikamilifu na hazijafungwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bwana Benson Mihayo amesema mwaka 2020/21 Halmashauri hiyo ilikaguliwa na kupata Hati safi ikiwa ni matunda ya ushirikiano kati ya Halmashauri, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na malelekezo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kuhakikisha wanaendesha Taasisi hiyo kwa mujibu wa Sheria.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.