Katibu Tawala Mkoa (RAS) Mkoa wa mwanza Christopher Kadio amehitimisha mkutano wa 14 wa kamati ya Ukaguzi wa madini (ICGLR) unao husisha nchi (12) za maziwa makuu, Mkutano huu umefanyika katika hoteli ya Belmont jijini Mwanza kwa lengo la kupambana na uvunaji haramu wa madini ili kuongeza thamani ya madini na kukuza uchumi wa nchi za maziwa makuu.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella Kadio ameupongeza ujio wa wanakamati hao mkoani hapa kwani wameweza kutembelea na kuzitangaza fursa za kitaliii zilizopo mkoani Mwanza pia amewakaribisha kutembelea fursa nyingine za kitalii zilizopo jirani kama Serengeti kwani ujio huu umesaidia kuutangaza mkoa wetu na kukuza uchumi wetu.
“Wageni wetu wamepata fursa pia wasaa wa kuweza kuangalia fursa za kitalii tulizonazo kama kisiwa cha sanane na utalii uliopo pia tumewaambia tuko jirani na maeneo ya utalii kama Serengeti wanaweza pia kuitembelea,” Alisema Kadio.
Aidha Kadio amebainisha kuwa licha ya kujaliwa na Mwenyezi Mungu maliasili nyingi lakini changamoto imekuwa maliasili tulizojaliwa zinawasaidiaje wananchi wa nchi zetu, pia amepongeza lengo la kamati hiyo kwani itasaidia kuhakikisha maliasili zinavunwa kwa njia sahihi na kuleta faida kwa wananchi wake.
“Nchi hizi zimejaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na maliasili nyingi lakini changamoto imekuwa maliasili tulizojaliwa zinawasaidiaje wananchi wa nchi zetu pia tunashukuru kwamba hii kamati ya ukaguzi inafanya sehemu yake katika kuangalia na kuhakikisha kuwa maliasili hizi zinapovunwa biashara hii ikiwa wazi tunaweza kuona wananchi wanapata faida katika biashara hii,” Alisema Kadio.
Naye Katibu Mkuu wa kamati hiyo Mhe. Barozi Zackary Muburi Muita ameweza kubainisha matokeo ya uvunaji haramu wa madini kwani unachangia vita na serikali kukosa mapato ya miradi ya wananchi wake.
“Sababu ya uvunaji haramu wa maliasili unachangia sana vurugu, vita na serikali kukosa utajiri wa miradi ya wananchi hasa madini,” Alisema Muita.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Fr. David Ngoy Luhaka amesema wameweza kuzindua kitabu kipya cha kamati hiyo kitakacho angalia madini yanachunguzwa katika njia ya uwazi na kusema kitabu hicho kipo wazi kwa kila mwanachama wa jumuiya hiyo.
“Tumeanzisha kitabu kipya kitakacho toa nafasi kwa wanachama wake wenye kampuni la ukaguzi wa madini kujiorodhesha ili kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara” Alisema Luhaka.
Aidha ametoa wito kwa nchi zote za Maziwa makuu ambazo hazijajiunga na kamati hiyo kuwa zinakaribishwa na mlango upo wazi kwani lengo kubwa ni kuhakikisha madini yetu yanathaminiwa katika hali nzuri.
“Niwatake kuwa nchi zinazotaka kuungana nasi katika uchunguzi mlango upo wazi hata kama kuna nchi mbalimbali waje kwa sababu tunapenda wote walio katika nchi za maziwa makuu ili madini yetu yathaminiwe katika hali nzuri,” Alisema Luhaka.
Hata hivyo Kadio ametoa ushauri kwa washiriki wa kikao hicho kwa kuwashauri pia kuwa waadilifu katika kamati hiyo ya ukaguzi kwani watasaidia katika kupiga hatua kwenye sekta hii ya madini lakini pia amewatia moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi zetu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.