JIJI LA MWANZA LAJIELEKEZA KWENYE MATUMIZI BORA YA ARDHI WAJENGA MADARASA MFUMO WA GHOROFA
Halmashauri ya Jiji la Mwanza yakamalisha Ujenzi wa Madarasa 12 kati ya 16 kwa mfumo wa ghorofa kwenye Shule ya Sekondari ya Mirongo kwa gharama za zaidi ya Sh Milioni 513.5 kutoka vyanzo vya Mpango wa Ustawi wa Taifa na Kuthibiti Uviko 19, mapato ya ndani ya Halmashauri na Serikali kuu.
Hayo yamebainishwa leo julai 15, 2023 wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika kuzindua madarasa 12 yaliyokamilika kwa awamu ya kwanza yakiwa na samani ambayo yatasaidia kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani kwani yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 600.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa madarasa hayo, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Ndugu Abdalla Shaibu Kaim ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kujenga madarasa kwa mfumo wa ghorofa ambapo yatasaidia kupunguza gharama za ujenzi kutokana na kutumia ardhi ndogo tofauti na endapo wangejenga kwa mfumo wa kawaida.
"Baada ya kukagua nyaraka na ujenzi kwa ujumla, Mwenge wa uhuru umeridhika na ubora na ndani ya siku tano naomba tuyafanyie kazi mapungufu hasa kwenye upande wa viti na meza ili vijana wapate elimu kwenye mazingira bora kabisa kama Mhe. Rais alivyoweka nia hiyo." Ndugu. Kaim.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyamaganawa Mhe. Amina Makilagi amefafanua kuwa kwa sasa wanafunzi watakaa kwa uwiano wa 50 kwa darasa tofauti na hali ilivyokua ambapo walilazimika kuketi wanafunzi 100 ndani ya chumba cha darasa jambo ambalo lilipelekea kuwa na mazingira magumu ya ufundishaji na kujifunzia kwa wanafunzi na walimu.
"Miaka 2 nyuma shule za ghorofa jijini Mwanza zilikua tatu tu lakini ndani ya Miaka Miwili ya Rais Samia tumejenga madarasa kwa mfumo wa ghorofa kwenye shule 13, achilia hapa lakini pale bugarika pakikamilika tutakua na madarasa 16, Mkolani, Mandu na Mkuyuni madarasa 24 kwa mfumo huu kwakweli tuwapongeze wote waliosimamia miradi hii." Mhe. Makilagi.
Awali taarifa ya radi huo iliyosomwa kwa mkimbiza Mwenge wa Uhuru ilifafanua kuwa uamuzi kwa Ujenzi wa madarasa hayo kwa mfumo wa ghorofa umetokana na hali ya ongezeko la watu na ufinyu wa ardhi na kwamba kwa ujenzi wa madarasa hayo 16 umeokoa eneo la ardhi la mita za mraba 656 na kwamba fedha zaidi ya milioni 88 zimeokolewa kwenye ardhi.
Mapema asubuhi, Mwenge wa Uhuru umekabidhi mifuko 300 ya saruji kwenye shule ya msingi Samia ambayo yatasaidia katika Ujenzi wa madarasa 10 yaliyoanzishwa na wananchi na baadae ukaangazia kwenye upande wa Sekta ya utawala ambapo umefanyika uzinduzi wa ofisi ya kata ya Mabatini.
Vilevile, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Unguja A kwa kiwango cha lami yenye urefu kwa mita 372 kwa gharama ya milioni 348.1 na kuagiza usimamizi mzuri ili ikamilike kwa ubora na wananchi wakatakiwa kutofanya biashara barabarani na kuhakikisha wanaitunza Miundombinu hiyo.
Kabla ya Mwenge wa Uhuru kufungua mradi wa ujenzi wa wa Miundombinu katika kituo cha afya Bulale na kuagiza urekebishaji wa mifumo ya maji na kutenganisha taa na feni ili mwanga usiwe na mawimbi, mwenge wa uhuru umeweka jiwe la nsingi kwenye jengo la uwekezaji la Family Corner linalojihusisha na makazi (Apartments).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.