KAMATI YA BUNGE YA TAMISEMI YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MIRADI YA ELIMU MWANZA
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI Mhe. Lazaro Nyamonga amesema kamati hiyo imeridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Uboreshaji Elimu ya Msingi (BOOST) na Sekondari (SEQUIP)
Mkoani Mwanza.
Mhe. Nyamonga ametoa pongezi hizo mapema leo tarehe 28, Oktoba 2023 wakati wa ziara ya Kamati hiyo mkoani Mwanza ambapo imebaini usimamizi mzuri wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri kwenye miradi ya Elimu uliofanikisha kukamilika kwa asilimia 100 kwa miradi ya BOOST na hatua ya Umaliziaji wa miradi ya SEQUIP uliofikiwa.
"Sisi kama Kamati tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi kwani tumeona mingi imeshakamilika na ambayo bado hasa ya Sekondari ipo kwenye hatua ya ukamilishaji na kwakweli tunampongeza Rais Samia kwa kutenga fedha nyingi kutekeleza miradi ya elimu" Makamu Mwenyekiti.
Aidha, Mhe. Makamu Mwenyekiti amewataka watendaji idara ya elimu kuongeza nguvu kwenye usimamizi wa miradi ya Ujenzi wa shule za Sekondari za wasichana nchini ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa kwani inatekelezwa kwa fedha nyingi zaidi ya Bilioni 4 kwa kila moja.
Naibu Waziri-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha nyingi kwenye utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa Elimu nchini ambapo amebainisha kuwa Kamati hiyo inakagua utekelezaji wa fedha hizo na namna Ilani ya CCM inavyotendewa haki.
"Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza zaidi ya Bilioni 7.9 kwenye uboreshaji wa Elimu ya Sekondari kupitia SEQUIP na zaidi ya Bilioni 12 kwa elimu Msingi kupulitia BOOST na sio Mwanza tu bali nchi nzima wanatekeleza adhma ya kupunguza umbali wa kufuata elimu." Mhe. Ndejembi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema miradi ya zaidi ya Bilioni 200 kwenye sekta ya elimu inatekelezwa mkoani humo na huku akipongeza miradi ya SEQUIP na BOOST ambayo mbali na ukarabati wa Miundombinu imewezesha ujenzi wa shule mpya katika maeneo mbalimbali.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martine Nkwabi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana TAMISEMI kwa kutekeleza miradi ya BOOST na SEQUIP mkoani humo ambayo inalenga kuwajengea walimu na wanafunzi mahiri katika nyanja mbalimbali zitakazoboresha matendo ya Kufundisha na kujifunza.
"Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za uboreshaji wa elimu kwani katika mwaka wa fedha 2022/23 Mkoa wa Mwanza umepokea jumla ya shilingi 7,940,016,756 kupitia programu ya SEQUIP Awamu ya II na Shilingi 12, 368, 100,000 kupitia BOOST" Nkwabi.
Aidha, amefafanua kuwa zaidi ya wanafunzi 8, 400 wa shule ya msingi wamepunguziwa umbali wa kutembea kufuata huduma ya elimu kwa kujengewa shule kwenye maeneo jirani na makazi yao na kwamba shule za msingi 59 zimeondokona na mlundikano wa wanafunzi madarasani kwa kuongezewa idadi ya vyumba vya madarasa katika shule hizo.
Kabla ya kukagua ujenzi wa Shule mpya ya msingi Ng'wang'hwalanga-Buhongwa B wilayani Nyamagana iliyojengwa kwa Milioni 540 (BOOST), kamati hiyo ilikagua ujenzi wa shule ya sekondari kata ya Kiseke - Ilemela inayotekelezwa kwa zaidi ya Milioni 584 (SEQUIP) ambapo imeiagiza halmashauri hiyo kuona namna ya kufidia eneo linalotarajiwa kujengwa kituo cha mafuta jirani na shule hiyo ili liwe la shule kwa ajili ya usalama wa wanafunzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.