**Maadhimisho ya Miaka 25 ya SAUT kwenda pamoja na kuanzishwa kituo cha Ubunifu cha Sayansi na Teknolojia*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amesema Maadhimisho ya mwaka huu ya Miaka 25 ya Chuo Kikuu cha Mt.Augustino SAUT yatakwenda pamoja na kuanzishwa Kituo cha Ubunifu cha Sayansi na Teknolojia ambacho kitakuwa mkombozi kwa maendeleo ya vijana hapa nchini.
Akizungumza leo Ofisini kwake katika Mkutano na Vyombo vya habari pamoja na uongozi wa chuo hicho Kikuu,Mkuu huyo wa Mkoa amesema ndani ya miezi miwili kituo hicho kitakuwa tayari kikijikita kwenye Kilimo,Uvuvi na Ufugaji na kitakuwa chuoni hapo.
Ameongeza kuwa tayari Serikali imeweka mazingira mazuri kwa vijana kwenye sekta ya Kilimo,Uvuvi na Ufugaji,hivyo kuwaongezea ujuzi zaidi kupitia kituo hicho kutaleta mapinduzi chanya katika maendeleo yao hasa kujiajiri wenyewe.
"Serikali ya Mkoa itatafuta maeneo kama pale shamba la mifugo la Mabuki tunaweza kuomba hekari kumi kwa ajili ya matumizi ya vijana kufundishwa Ufugaji bora na wa kisasa wa ng'ombe pia tutazishirikisha baadhi ya Halmashauri kutupatia maeneo rafiki ya Uvuvi na Kilimo,Amesisitiza Mhe. Malima.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha hatua hii itakiingiza Chuo cha SAUT kwenye sura ya kimataifa zaidi kwani mpango kama huu wa ubunifu umefanyika kwenye vyuo vingi maarufu Duniani kama Chuo Kikuu cha Havard kilichopo Marekani.
"Mhe.Mkuu wa Mkoa nakuahidi yote uliyozungumza tunakwenda kuyatekeleza hasa hili la kuanzishwa hiki kituo,Wataalamu wa kufanya kazi hii wapo na kila kitu kitakwenda sawa na kukamilika kwa wakati,"Mhe.Balozi.Prof.Costa Mahalu,Makamu Mkuu wa SAUT.
Kilele cha Maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo Kikuu cha Mt.Augustino kitakuwa ni Novemba 11,2023 huku shughuli mbalimbali za ndani na nje ya Chuo hicho kuelekea Maadhimisho hayo zikianza Mei mwaka huu
SAUT kilianza kuwa Chuo Kikuu mwaka 1998 awali kilijulikana kama Nyegezi Social Training Centre.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.