Akizungumza na waandishi wa habari katika banda lake kwenye maonesho ya wakulima Nanenane-Nyamhongolo mkoani Mwanza, Meneja Masoko wa Kampuni ya uuzaji na usambazaji wa zana za kilimo ya Kirasa Co.Ltd, Omari Msisi alisema kama wadau wa kilimo wamefurahishwa na hatua hiyo ambayo itatoa fursa kwa wakulima na wafanyabiashara kuwekeza sekta ya kilimo.
Msisi alisema kama wasambazaji wa zana za kilimo wamepokea kwa mikono miwili mpango wa Serikali kuja na uwekezaji mkubwa katika kilimo kitendo ambacho kitasaidia wakulima kutumia teknolojia katika kufanikisha kilimo cha biashara.
Msisi alisema kampuni ya Kirasa Ltd wamekuwa washirikiana na Serikali katika kufanikisha sekta ya kilimo, hivyo wamelazimika kupunguza gharama za matrekta yao aina ya Massey Furguson kwa sababu wameondolewa VAT ambapo aliwataka wakulima kuchangamkia fursa hiyo.
“Tumeamua kuleta trakta za kilimo za Massey Furguson ambazo zinatumika kila msimu kwa kubadildihiwa matumizi, wakati wa masika zitatumika kwa kulima mashamba, pia kiangazi zinatumika kusombea mizigo ikiwamo mchanga, tofali au mazao, vile vile zinatumika katika kusaga vyakula na kumwagilia maji kama utalima kiangazi.
“Kutokana na hali ya hewa kubadilika kila msimu, ni vema wakulima wakajikita katika kilimo cha kisasa kikiwamo cha green house na umwagiliaji, Tanzania badi tuna ardhi kubwa lakini tatizo letu tunalima kwa kuhama hama badala ya kutumia eneo dogo kwa kufuata kanuni na mbegu bora, sijajua kama tatizo ni elimu kushindwa kufika kwa wananchi.
“Tunawaomba wananchi wa kanda ya Ziwa na wale wanaofanikiwa kufika hapa Nyamhongolo waje hapa ili tupeane maelezo ya kutosha ikiwamo bei ya trekta, tunaweza kukukopesha na ukafanyia kazi na kulipa kidogo kidogo, lengo letu ni sawa na mpango wa Serikali kuona kilimo kinawanufaisha wakulima,”alisema.
Awali,Serikali ilisema sera iliyopo ya sekta ya kilimo inayotumika kwa sasa ndiyo cha chanzo cha wakulima kuwa masikini kutokana na kuwatumikisha wananchi kuilisha nchi na matajiri huku wakiwa wanakabiliwa na changamoto kubwa.
Kutokana na hali hiyo ilisema sera hiyo imepitwa na wakati ambapo wizara ya kilimo imelazimika kuanza kuipitia upya na kuondoa changamoto na vikwazo kwa wakulima ikiwa lengo ni kuihuisha sekta hiyo kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa cha biashara kwa kuruhusu uwepo wa uwekezaji mkubwa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akifungua sherehe za wakulima na maonyesho ya kilimo (Nanenane) katika viwanja vya Nyamhongolo mkoani Mwanza ambapo aliwapiga marufuku wakuu wa wilaya na mikoa kuwazuia wakulima kuuza chakula chao kwa kuhofia uwepo wa njaa.
“Hatuwezi kujenga viwanda wakati wakulima ni masikini wa kutupwa, ni lazima tuwawezeshe kwa kutengeneza mazingira ya watu kunufaika na kilimo chao sambamba na kuwa na soko la uhakika, ndio maana leo hii kama wizara tumeanza kupitia sera ya kilimo na kuondoa changamoto na vikwazo vilivyokwekwa .
“Sera iliyopo imepitwa na wakati kabisa, inawaumiza wakulima na kuwafanya kubaki kila mwaka kuilisha nchi na matajiri huku wao wakibaki na umasikini wao huku kukiwapo na utitiri wa taasisi nyingi ambazo ukichunguza zimeanzishwa kwa lengo la kuwakandamiza wakulima, hii haiwezekani kama wizara tumeanza kuangalia ni taasisi gani zinatkiwa kufutwa na kubaki chache .
“Fedha ambazo zilikuwa zikielekezwa kwenye utitiri wa taasisi hizo, zitaelekezwa katika mfuko maalum amboyo wizara tunatarajia kuanzisha na kazi ya mfuko huo ni kufidia mkulima pale inapotokea mtikisiko wa bei katika soko la dunia, kama serikali hatuna uwezo wa kuthibiti bei ya soko la dunia lakini mfuko huo ndio utakaokuwa na kazi ya kutafuta pesa kwa ajili ya kuwafikia wakulima,”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.