Madereva daladala na makondakta watakiwa kuthamini afya zao kwa kuona umuhimu wa kuwa na bima ya afya na kunufaika na huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu ili kuendelea kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa bidii na kuchangia uchumi wa familia zao na Taifa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mary Tesha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella wakati akikabidhi kadi za bima ya afya kupitia mfuko wa NHIF kwa wanachama wa Chama cha Madereva na Makondakta wa Daladala Mkoa wa Mwanza (MWAREDDA).
Alisema Taifa linahitaji watu wenye afya ili kufanya mambo ya kimaendeleo hivyo ni bora kutokusubili mpaka kuugua jambo la msingi ni kupima na kuanza matibabu kabla ugonjwa haujawa mkubwa hiyo itasaidia kuepukana na vifo vya gafla .
"Watu wote tupo kwenye hatari ya kupata ajali lakini hili kundi lenu lipo kwenye hatari zaidi kwa sababu muda mwingi mpo barabarani hivyo bima ya afya ni muhimu pindi upatapo ajali upate matibabu bure nasikia kuna watu wanafia kwenye gari wakiwa wanaendesha hiyo kwa sababu hakujua kama anaumwa na inatokana na kutokupima na kutojihusisha na masuala ya afya,"alisemaTesha.
Naye Mwenyekiti Msaidizi MWAREDDA Ezekiel Lameck alisema wao wapo tayari kuwekeza kwenye afya japo kuwa vipato vyao siyo vya kuridhisha lakini wanatambua kuwa bila ya kuwa na afya bora hawataweza kumudu kazi yoyote na kuwa rahisi zaidi kupoteza maisha .
Aliongeza kuwa chama hicho kilianzishwa mwaka jana kikiwa na wanachama 50 ambapo hadi sasa kina wanachama 320 hivyo lengo ni kuhakikisha wanachama wote wanajiunga na mfuko wa NHIF ili kuondokana na adha ya kupata huduma za matibabu.
“Lengo la kuanzishwa kwa chama hiki ni kutetea haki na wajibu wa madereva na makondakta katika kazi zao, kutoa elimu na kuwajengea uwezo ili waweze kumudu vyema majukumu yao kwa mjibu wa sheria za nchi hususani sheria za usalama barabarani pamoja na kupigania mazingira bora ya kazi zao,”alisema Lameck.
Kwa upande wake Kaimu Meneja mfuko wa NHIF Mkoa wa Mwanza, Calystus Mpangala amesema kwa mwaka wa fedha 2017/18 malengo yalikuwa kusajili wajasiriamali 1200 Mkoani Mwanza kupitia mpango wa KIKOA ambapo hadi sasa umevuka lengo kwa kusajili wajasiriamali 1,223 hii ikiwa ni sawa na asilimia 102.
Aliongeza mfuko wa bima ya afya umedhamiria kumfikia kila mtanzania hivyo bodi imeridhia kuwa na utaratibu wa utoaji huduma za matibabu kwa kadi kwa vikundi ama ushirika vilivyo katika sekta isiyo rasmi kama mama lishe,AMCOS, SACCOS, VICOBA, umoja wa bodaboda na daladala na kundi la ujasiliamali ambao hawawezi kugharamia matibabu kama watu binafsi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.