Madereva waaswa kutumia Ujuzi, Weledi kuzuia Ajali za barabarani
Madereva Wakuu na Maafisa Usafirishaji kutoka Kanda ya ziwa wameaswa kutumia vizuri Mafunzo wanayopata kupunguza ama kuondoa moja kwa moja ajali za barabarani kwa kuwasaidia madereva wengine katika kufahamu namna bora ya kusimamia vyombo vyao vya usafiri.
Wito huo umetolewa mapema leo jumatatu tarehe 21 Agosti, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla alipokua akifungua Mafunzo ya siku tano yanayotolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kwa Kundi hilo.
Mhe. Ngaga amesema mafunzo wanayotapata yawe chachu kwa madereva wote kwenye taasisi za umma na hata binafsi kwenye kudhibiti ajali za barabarani na matumizi makubwa ya rasilimali kama mafuta na fedha ambazo kwa ujumla limekua eneo nyeti kwenye ofisi za umma.
Vilevile, ametoa rai kwa kundi hilo na hata jamii kwa ujumla kutumia chuo cha Taifa cha Usafirishaji kujiendeleza kielimu kufuatana na wakati hususani kujibidiisha kwenye eneo la teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha wanaendelea kuvifahamu vyombo vya usafiri vya kisasa na kuweza kuvitumia.
"Ni Imani yangu kuwa washiriki wote mkitoka hapa mtakua mabalozi wazuri kwa jamii kukisemea chuo chetu kuwapeleka Vijana wao kupata ujuzi na elimu kwani wanatoa kozi mbalimbali sio tu za ufundi kama ilivyozoeleka kwa miaka mingi kwenye jamii." Mhe. Mkuu wa Wilaya.
Naibu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Dkt. Prosper Mgaya ametumia wasaa huo kuwasihi washiriki kutumia mafunzo hayo kupata ujuzi ambao utasaidia kuipunguzia gharama za uendeshaji na rasilimali kama mafuta na fedha na akatoa wito kwa jamii kwenda kwenye chuo hicho kupata ujuzi.
"Mhe. Mgeni rasmi , Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kinaendesha kozi nyingi ikiwemo Ile ya mafunzo ya Anga ambayo inafadhiliwa na Benki ya Dunia hivyo mtu yeyote akija kusoma atapata mafunzo bila malipo na ndio wafadhili wa mafunzo haya ambayo yanaendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini." Amefafanua Naibu Mkuu wa Chuo.
Akimkaribisha Naibu Mkuu wa Chuo, Mkuu wa Idara ya Kituo cha Mafunzo Ueledi Ndugu Bahati Mabina amebainisha kuwa washiriki 103 kutoka mikoa mbalimbali ya kanda ya ziwa watapatiwa mafunzo mahiri kwa siku tano ambayo yatawabadilisha kiutendaji kutokana na ujuzi watayoyapata.
"Baada ya mafunzo haya mwisho wa siku Maafisa usafirishaji watalifahamu Gari vizuri ambapo itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa magari na kuipunguzia mzigo serikali na hata kupunguza ajali barabarani kwani watajengewa uwezo kwenye eneo la Maadili na uadilifu." Amesema Bahati Mabina.
Maafisa usafirishaji na madereva wakuu kutoka taasisi za Umma kutoka mikoa ya kanda ya ziwa watajengewa uwezo kwenye maeneo ya matengenezo ya magari, tabia za madereva na usimamizi wa mafuta, Ukaguzi wa Magari na kubaini hitilafu, umakini kwenye matumizi ya matairi na Itifaki ya kuwaendesha viongozi kwa siku 5.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.