Mafunzo ya Umiliki Manufaa yana tija kwa Mkoa wa Mwanza ambao ni kitovu cha Biashara-RAS Mwanza
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana leo januari 06, 2024 amefungua mafunzo ya Umiliki Manufaa kwa wataalamu wa sheria na kubainisha yamekuja wakati mwafaka kwa Mkoa huo ambao ni kitovu cha biashara na unaokuwa kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba yake kwenye ukumbi wa mikutano Hotel ya Victoria Palace, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu, Daniel Machunda amewapongeza waandaaji wa mafunzo hayo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni,BRELA kwa kuwa na lengo la kuhakikisha huduma bora zinatolewa na kupatikana kwa urahisi.
Amesema Mkoa wa Mwanza upo kimkakati kutokana na kupakana na nchi za maziwa makuu kufanya kuwepo na fursa kubwa ya kibiashara,hivyo mafunzo hayo yatakuwa na tija kwa wafanyabiashara kwa kufuata miongozo sahihi na mwishowe kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
"Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto za taarifa za baadhi ya wamiliki ambao wanaweza kutumia Makampuni yao kukwepa Kodi au kupitisha fedha haramu,"amesema Machunda wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia vizuri nafasi hiyo na kuwa mabalozi kwa wengine na kuwepo na muendelezo mzuri wa utoaji wa huduma bora.
Kwa upande wake Afisa Sheria Mkuu wa BRELA,Menrad Rweyemamu amesema Taasisi hiyo siku zote imesimama imara kuhakikisha miradi kutoka ndani na nje ya nchi inaingia kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.