Leo Septemba 13, 2022, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amezindua Jengo la kisasa la ghorofa tano la Huduma za Mama na Mtoto kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure Mwanza lililojengwa kwa Zaidi ya Bilioni 12.
Akizungumza na wananchi kwenye hafla ya Uzinduzi wa Jengo hilo, Dkt. Mpango ameipo geza Wizara ya Afya, Uongozi wa Mkoa, na Hospitali hiyo pamoja na Mkandarasi aliyejenga Wakala wa Majengo nchini (TBA) kwa kazi nzuri ambayo itasaidia kuboresha huduma na kusaidia kupunguza Vifo vya Mama na Mtoto na vifo vitokanavyo na Uzazi.
Dkt. Mpango amesema uwepo wa jengo hilo ulioenda sambamba na ufungaji wa vifaa vya kisasa kama vya uchunguzi wa Magonjwa kwa kutumia Mionzi na Kipimo cha moyo, umetokana na ukweli kwamba mahitaji ya huduma za mama na mtoto mkoani humo yameongezeka na kwamba Serikali inaendelea kuboresha huduma hizo nchini kote.
"Muswada wa Bima ya Afya kwa wote nchini utawasilishwa kwenye vikao vya Bunge vinavyoanza leo, ninaitaka wizara ya Afya kuendelea kufanyia kazi changamoto zote zinazoukabili mfuko wa Bima ya Afya nchini ili uendelee kutoa huduma bora kwa wananchi kwani kila mwananchi anayo haki ya kupata huduma bora za Afya tena karibu na eneo alilopo." Amefafanua Dkt. Mpango.
Aidha, ametoa rai kwa wataalamu wa Sekta ya Afya kutoa Elimu ya Uzazi kwa wazazi wote kuhusu lishe bora na kutojihusisha na matendo maovu ambayo ni kinyume na Maadili ya kazi ya Utabibu na amewataka akina baba kusaidia wake zao wakati wote wa kabla, wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua kwa malezi ya mama na mtoto baada ya kujifungua.
Dkt. Mpango ametoa wito kwa uongozi wa Mkoa kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kufanya Usafi wa mazingira na wananchi wote waweze kutambua kuwa Usafi wa mazingira ni Afya na ni jukumu la kila mmoja kufanikisha kampeni ya Kitaifa ya kuweka mazingira safi nchini inafanikiwa ili kuiepusha jamii na maradhi yatokanayo na uchafuzi wa mazingira.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Afya Mhe. David Mollel amemshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutumia fedha za Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 kwenda kuhudumia wananchi kwa kuwaletea vifaa vya kisasa kama CT Scan za Kisasa kwenye Hospitali zote za Mikoa ambazo zimesaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
"Tunatoa pongezi za dhati sana kwenu kwa nia njema ya kupunguza vifo vya Mama na Mtoto kwa kuboresha huduma za Afya nchini kwani ukitazama bajeti nzima ya TAMISEMl utaona zaidi ya Trilioni 2.5 zimetengwa kwenda kuhudumia wananchi, hongereni sana." Mhe. Stansilaus Nyongo (MB), Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amefafanua kuwa, Mkoa huo umepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 37 kwenye sekta ya Afya na kwamba zinajenga Vituo vya Afya 10 na zaidi ya Zahanati 100 kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Serikali Kuu na kufanya ongezeko la vituo vya afya 22 kutoka 10 vya awali na hali ya Chanjo ya Ugonjwa Uviko 19 imevuka malengo.
Mganda Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure, Bahati Msaki amefafanua kuwa uzinduzi wa jengo hilo unaenda sambamba na ongezeko la vitanda kufikia zaidi ya 500 kutokana na uwepo wa Vitanda vipya 261 na kutakua na huduma za kisasa za kipimo cha Moyo kinachotumia umeme, Maabara, uchunguzi wa magonjwa yatokanayo na mfumo wa Chakula pamoja na vipimo vya Tumbo, Kizazi, mishipa viungo kama Matiti na vipimo vya Kichwa, kifua na shingo kwa mashine ya kisasa ya CT Scan.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.