Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, Mheshimiwa Anne Makinda amewashauri wasomi na Wananchi Nchini kutumia takwimu za sensa ya watu na Makazi katika kubuni biashara ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Makinda ametoa ushauri huo leo Machi 29, 2023 wakati akizungumza na wananchi pamoja na viongozi kutoka makundi mbalimbali Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza kuhusu matumizi ya Matokeo ya Sensa ya watu na Makazi 2022 katika kupanga na kutekeleza Mipango ya Maendeleo.
Amesema Serikali haikufanya sensa ili takwimu hizo zikae kwenye shelfu zake bali ziwasaidie watanzania kuona fursa ili wazitumie kujikwamua kiuchumi wao na taifa kwa ujumla.
Amesema kwa mujibu wa sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zaidi ya nusu yao ni kundi lenye uwezo wa kufanya kazi hivyo wote wakishiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi watajikwamua wao, familia zao na taifa kwa ujumla.
"Tuanze kufikiri kitakwimu badala ya kufanya kazi kama watu tuliofungwa kitambaa usoni, sensa iwafungue wasomi na vijana kuona fursa, fanyeni biashara na dunia nzima kimtandao.
"Fursa zinakwenda na wakati hazirudi mara mbili ukichelewa zitakuacha wasomi acheni kuchagua kazi kikubwa ninachoweza kuwashauri kuweni waaminifu tatizo letu asilimia kubwa si waaminifu kama tukiendelea kufanya kazi kwa udanganyifu kama ambavyo wengi wetu walivyozoea itakula kwetu," amesema Mheshimiwa Makinda na kuongeza.
"Ukichagua kazi hautapata kazi mpaka utastaafu(utazeeka) kabla ya kuajiriwa,"amesema.
Akizungumzia kuhusu takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mheshimiwa Makonda amewashukuru watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa hali iliyosaidia zoezi hilo kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Hassan Masala amesema Wilaya hiyo ilitekeleza zoezi la sensa kwa heshima na umakini mkubwa ndiyo maana wamepata fursa ya kuwa miongoni mwa maeneo ya mfano ambayo Kamisaa Makinda amewapendekeza kuyafikia.
"Wilaya ya Ilemela tulitekeleza zoezi la sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka jana kwa weledi mkubwa na tuko tayari kuyafanyia kazi maelekezo yote utakayotoa leo,"amesema Mheshimiwa Masala
Naye Meneja Takwimu wa Mkoa wa Mwanza, Goodluck Lyimo amesema asilimia kubwa ya wakazi wa mkoa huo walijitokeza kuhesabiwa hali iliyosaidia kufanikisha zoezi hilo kwa kiwango kikubwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.