MELI YA KISASA YA MV MWANZA KUNUFAISHA NCHI ZA MAZIWA MAKUU : RC MAKALLA
*Asema majaribio ya mitambo kwenye Meli hiyo yanakwenda vizuri*
*Abainisha kesho kusainiwa mkataba wa ujenzi Jengo la abiria uwanja wa Ndege*
*Ujenzi wa Hoteli, upanuzi uwanja kuwa Kimataifa ni mikakati kukuza Utalii*
*Balozi asifu juhudi za Serikali kuunganisha Watanzania na Waganda*
*Balozi akaribisha Wafugaji, Wakulima na Wavuvi kujifunza Uganda*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amesema kukamilika kwa ujenzi wa Meli kubwa ya kisasa ya MV Mwanza HKT pamoja na miradi mingine ya kimkakati ya uchukuzi kutaongeza wigo wa usafirishaji wa bidhaa kwa nchi za maziwa makuu
Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 27, 2024 wakati wa kikao kifupi na Mhe. Meja Jenerali Balozi Paul Simuli, Balozi wa Tanzania nchini Uganda kilichofanyika Ofisini kwake kufuatia ziara ya kikazi ya Balozi huyo mkoani Mwanza kwenye miradi ya kimkakati ya Reli ya kisasa pamoja na Meli hiyo.
"Juzi tumeanza majaribio ya mitambo kwenye ujenzi wa Meli yetu ya kisasa ya MV Mwanza na chombo kipo sawa, kilichobaki ni kufunga viti na vitanda kwenye meli hiyo na ikianza kazi basi nchi ya Tanzania na Uganda zitakua karibu sana maana itafika huko na kwenye mataifa mengine", amefafanua.
Vilevile, Mhe. Makalla amebainisha kuwa Serikali imedhamiria kuufanya uwanja wa ndege Mwanza kuwa wa Kimataifa na kwamba Machi 28, 2024 watasaini mkataba wa ujenzi wa jengo la abiria pamoja na kupanua sehemu ya uwanja huo ili mataifa ya nje yatue na kupaa moja kwa moja Mwanza
Naye, Mhe. Meja Jenerali Balozi Paul Simuli, Balozi wa Tanzania nchini Uganda amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa usimamizi wa miradi ya kimkakati ambayo Mhe. Rais amekua akihakikisha inatekelezwa ili kuwaletea wananchi maendeleo hususani kwenye sekta ya uchukuzi.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwakaribisha Wakulima, Wavuvi na Wafugaji kutoka Mkoani Mwanza ili waweze kwenda Uganda kujifunza namna bora ya kuboresha sekta hizo mathalani eneo la Uvuvi kwa kutumia vizimba ambalo litasaidia kuondoa upungufu wa Samaki kwenye ziwa Victoria.
Katika wakati mwingine, Makalla ameupokea uongozi UWT Taifa ukiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Marry Chatanda ambao wanaotarajia kuwanoa wanawake waweze kugombea nafasi mbalimbali kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.