Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima amesema Serikali inaendelea kutekeleza Miradi ya Maendeleo kwa ufanisi Mkubwa mkoani humo ikiwemo na Miradi ya Kimkakati kama ya Ujenzi wa Meli ya kisasa ya MV Mwanza na Daraja la Kigongo- Busisi ikiwa ni kutokana na Mtiririko Mzuri wa fedha za wakandarasi na kwamba hakuna mradi uliosimama.
Amesema hayo leo jumatano ya Machi 15, 2023 kwenye Ukumbi wa Chuo Cha Fedha (BOT) Mkoani wakati wa kongamano la kuangazia utekelezaji wa shughuli za Serikali zilizofanywa kwa kipindi cha Miaka Miwili chini ya Uongozi Rais Samia Suluhu Hassan ambapo viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi zisizo za Serikali pamoja na wananchi wameeleza hisia zao juu ya uongozi huo mahiri.
"Lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuleta fedha hizi zote ni kuboresha viwango vya maisha ya kila Mtanzania na kwakweli nchi hii imefanikiwa sana kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi wake." Amesema Malima.
Akizungumzia suala la huduma za Maji kwa wananchi Mhe. Malima amebainisha kuwa Mhe. Rais ameleta zaidi ya bilioni 70 kutekeleza Mradi Mkubwa wa Maji wa Butimba ambao utakapokamilika unatarajia kuzalisha zaidi ya Lita Milioni 48 kwa siku na kwamba mradi huo utasaidia kuondoa adha ya maji hasa kwa wananchi wanaoishi kwenye miinuko kwenye jiji hilo.
"Juhudi kubwa sana zimefanywa na Serikali ya awamu ya Sita kama kuimarisha Kitengo cha ukusanyaji fedha (TRA) na kuminya Mianya ya Upotevu wa fedha na kufanya ongezeko la zaidi ya Bilioni 500 kwenye ukusanyaji wa fedha kwakweli tunampongeza sana Mhe Rais kwa hili." Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mhe. Sixbert Jichabu.
"Rais Mama Samia Suluhu Hassan ametupa furaha na kuamua kutoa msimamo wa viwango bora vya kutoa Elimu kwa kuboresha na kuimarisha Elimu kwa kuweka mazingira rafiki ya ili elimu yetu iwe bora kwa kila mtanzania na vilevile tunampongeza kwa kutujengea barabara zetu." Amesema, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu
Mkurugenzi wa Kampuni ya huduma za Meli (MSCL) Mhandisi Eric Hamissi ameipongeza Serikali kwa kasi ya kutoa fedha za Miradi na amebainisha kuwa mradi wa ujenzi wa Meli ya MV Mwanza unaogharimu zaidi ya Bilioni 109 umefikia asilimia 82 hata hivyo amegusia fursa ya kusafirisha mizigo inayokuja siku za usoni kutokana na Ukarabati wa MV Umoja kwa Bilioni 19 inayobeba zaidi ya Makontena 21 kufikia asilimia 72.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa Mhandisi Paschal Ambroce amefafanua kuwa awali Ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye thamani ya zaidi ya Bilioni 700 ulifikia asilimia 24 lakini kutokana kasi nzuri ya kutoa fedha, mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 70 ya Utekelezaji kwa sasa.
Meneja TARURA Mkoa amesema ndani ya miaka miwili ya Rais Samia Serikali imeongeza bajeti kwenye miradi ya barabara mkoani humo kutoka Bilioni 10.5 miaka ya 2021/22 hadi Bilioni 26 na kwamba kutakua na ongezeko la zaidi ya KM 22 za Lami kutokana na ongezeko hilo.
Kwa upande wake Mhandisi Godfrey Sanga Meneja RUWASA Mkoa amebainisha kuwa wananchi kupitia taasisi hiyo wananufaika na Miradi ya Maji yenye thamani ya Bilioni 157 tofauti na awali ambapo Serikali ilitenga bajeti ya Bulioni 13 pekee na kwamba hali hiyo imesaidia kuongeza hali ya Upatikanaji wa Maji kutoka asilimia 65 hadi 89.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Ugavi wa Umeme amebainisha kuwa zaidi ya Bilioni 78 zimetolewa ndani ya miaka miwili kutekeleza miradi ya Umeme vijijini ambayo imewafikia zaidi ya wananchi 24721 na kwamba Taasisi hiyo kwa sasa wanatumia mfumo wa kidigitali ambao umesaidia kuwahudumia zaidi ya wateja Elfu 20 ndani ya siku sita tu.
Vilevile, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kwimba Emmanuel Sherembi amejinasibu kwa kuletea fedha za kujenga Shule mpya ya Sekondari wilayani humo yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 3 na kwamba amebainisha kuwa zaidi ya Bilioni 23.1 zimetolewa ndani ya miaka miwili kwa ajili ya Utekelezaji wa Miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, Maadhimisho hayo yamepata fursa ya kufahamu kuwa ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita zimeletwa fedha za kukamilisha Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ilemela na kwamba Manispaa hiyo imepokea zaidi ya Bilioni 45 huku Kwimba ikipokea Bilioni 28 za kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo.
Nao, wafanyabiashara wadogo (Machinga) wamempongeza Mhe. Rais kwa kuwatambua na kuwapangia maeneo rasmi ya kufanya biashara zao huku Bakari Kadabi Mwenyekiti wa Wavuvi nchini amesema wanafurahia sekta yao kutokana na Utaratibu mzuri wa kazi na mwisho Sheikh Mussa Kalwanyi akitumia jukwaa hilo kutoa wito kwa wananchi kulinda amani ya nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.