Wananchi wa Wilaya ya Misungwi leo Julai 25, 2022 wameungana na Mhe. Mkuu wa Mkoa katika Kuchimba Misingi ya Ujenzi wa Madarasa 24 kwenye shule ya Msingi Mbela ikiwa ni ishara ya Uzinduzi wa kampeni kubwa ya kizalendo ya Ujenzi wa Miundombinu ya Madarasa kwa shule za Msingi na Sekondari Mwanza.
Akizungumza na mamia ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amesema kampeni kubwa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ni matokeo ya mawazo ya viongozi wote ndani ya Mkoa wa mwanza kwa kiu ya kutaka kuona watoto wanasoma kwenye mazingira rafiki na kwamba kazi hiyo itafanywa kwenye kila Halmashauri huku ikihitaji Madarasa 11904 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 230.
"Nawashukuru sana wananchi wa Misungwi, huu ndio Uzalendo maana kampeni hii ina thamani ya Bilioni 230 kwani tunahitaji kujenga zaidi ya vyumba 11900 vya madarasa lakini kwa kazi hii tumeokoa fedha nguvu kazi na pale zinapohitajika fedha basi tutatumia fedha na tunajenga vyumba 52 hapa maana mtoto akikaa kwenye msongamano au chini hawezi kuandika vizuri." Mkuu wa Mkoa.
Niwashukuru wananchi kwa kujitokeza kuchimba msingi, kusomba mawe, Maji na Mchanga kuchangia nguvu kwenye ujenzi huu maana zoezi hili ni la kizalendo na hapa pamoja na kupata madarasa ya nyongeza kwenye shule mama tutapata shule mpya hapa ambayo kwa kuanzia tunajenga madarasa 15, tuendelee na moyo huo. Mkuu wa Wilaya ya Misungwi.
"Kwenye Jimbo hili shule hii ndio yenye wanafunzi wengi zaidi kuliko zingine zote, uwezo wa shule yetu hii ni wananfunzi 700 lakini ina zaidi ya wanafunzi 2900, madarasa haya yakikamilika yatakua suluhisho la kudumu, tunakushukuru sana Mhe. Mkuu wa Mkoa na usiache kutusaidia." Mbunge wa Misungwi, Mhe. Alexander Mnyeti.
"Nimesikia kilio cha shule ya Msingi Mbela na ndio maana leo nipo hapa leo kuwaunga mkono wananchi na viongozi wa Mwanza kwa jambo hili la kizolendo la kujenga vyumba vya madarasa kwa sababu ya upungufu mkubwa, nimeamua kuchangia matofali 400 kwenye kila wilaya kwa shule yenye upungufu mkubwa wa Madarasa." Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Mhe. Kabula Shitobelo
Bi. Leticia Joseph Mkazi wa Ufundi Misri amesema yeye kama Mzazi mwenye watoto wawili kwenye shule ya Msingi Mbela ana furaha kwa Kampeni ya Ujenzi wa Vyumba vya Madarasa huku akibainisha kuwa awali kulikua na changamoto ya madarasa hali inayosababisha wanafunzi kupokezana Madarasa kwa zamu kwa wiki wakienda asubuhi na inayofuata wakiingia mchana.
"Viongozi wa Vijiji hadi Mkoa tupo nao pamoja kwenye harakati hizi zinazoenda na Kaulimbiu ya Uzalendo kwanza, Kazi na Iendele na hapo baadae tunataka tuwe na Sekondari maana hapa kwetu Misungwi tuna upungufu hata wa shule za Sekondari. Amesema Mzee Hamis Mtoro kutoka Mtaa wa Bomani.
Philipo Manumbu, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Misri amefafanua kuwa katika kijiji cha Mbela kuna shule moja tu ya msingi kwa Vitongoji sita na ndio maana ina zaidi ya wanafunzi 2900 hivyo ameshukuru wananchi kuiunga mkono serikali kwa kujitokeza kwa wingi kuchimba Msingi wa Ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwamba baada ya Uzinduzi huo zoezi litakua endelevu.
Pamoja na michango hiyo ya wananchi, viongozi na Ofisi mbalimbali wametoa nguvu mchango wa Saruji, Matofali, Bati, Mchanga, Chakula na Mbao katika kuhakikisha kampeni yenye Kaulimbiu Uzalendo kwanza, Kazi na Iendelee inafanikiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.