Jumla ya Shule Mpya 11 na vyumba vya madarasa 983 vinatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu Mkoani Mwanza tayari kwa ajili ya kutumika na wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaoanza masomo mwaka 2023.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza Mwalimu Martin Nkwabi akizungumza leo Ofisini kwake na Vyombo vya Habari amesema Mkoa huo umepokea zaidi ya Shs Bilioni 19 ambazo zimeelekezwa kukamilisha ujenzi huo.
"Tangu kuanza mpango wa elimu bure mwaka 2016 Mkoa wa Mwanza umevunja rekodi tangu kupata Uhuru kwa kuwa na idadi ya wanafunzi 105,864 waliohitimu Elimu ya Msingi mwaka huu," amesema Afisa Elimu.
Mwalimu Nkwabi amebainisha kuwa kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza zinajengwa Shule hizo ambazo kila moja itagharimu Shs Milioni 600 na zingine tayari zimepata usajili.
"Tumejipanga vizuri kwa ajili ya wanafunzi hao hata kama wote watafaulu uwezo wa kusoma katika mazingira bora upo kutokana na mkakati uliopo wa kuboresha sekta ya elimu Mkoani hapa," amesisitiza Nkwabi
Aidha, amesema Mkoa huo umejenga Shule ya kisasa ya Sekondari ya Wasichana Wilayani Magu itakayochukua wanafunzi elfu moja kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita iliyogharimu Shs Bilioni 4 ambayo itakamilika kabla ya Disemba 15 mwaka huu.
Nkwabi ametoa rai kwa Maafisa elimu wote Wilayani kuhakikisha wanasimamia kwa weledi miradi hiyo ya ujenzi kwa kujiridhisha imekuwa na ubora kabla ya kuruhusu malipo kufanyika.
Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8000 nchi nzima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.