Ofisi ya Waziri Mkuu ,Kazi ,Vijana, Ajira na wenye ulemavu imefanya Mkutano wa siku moja jijini Mwanza katika ukumbi wa BOT wenye lengo la kukusanya maoni ya vijana, ya kuhuisha Sera mpya ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ambapo vijana wapatao 150 kutoka Mikoa mbalimabli ya Tanzania wameshiriki.
Akifungua Mkutano huo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Bw.James L. Kajugusi amewashukuru viongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuwakaribisha na kutoa huduma katika kufanikisha Mkutano huo, Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha kwamba zoezi la mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 linaendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa na washiriki wote kwa kukubali kushiriki mafunzo hayo.
Bw.Kajugusi ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeamua kufanya mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 kwa sababu, Idadi ya vijana ambayo ndio rasilimali muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kuongezeka sana ukilimganisha na ukosefu wa ajira, masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yanayojitokeza ambayo yanapelekea kuwepo haja ya kufanya mabadiliko yanayozingatia idadi ya vijana waliopo nchini na mahitaji yao katika kila sekta.
“Vijana kutoka milioni 11.7 mwaka 2002 hadi kufikia milioni 16.1 mwaka 2012 na mahitaji na changamoto za vijana nchini pia yamekuwa yakiongezeka kiasi cha kupelekea kuwepo kwa haja ya kufanya mapitio ya Sera iliyopo sasa ili idadi na nguvu ya vijana itumike vizuri”,alisema Kajugusi, kwa kuzingatia fursa za maendeleo zitokanazo na ukuaji wa Sayansi na teknolojia, vipaumbele vya kitaifa na Kimataifa ikiwa ni pamoja na vijana kushiriki kikamilifu katika kutekeleza malengo Endelevu ya Dunia(SDG’s) ifikapo mwaka 2030.
Aidha ameongeza kuwa, sababu hizo pamoja na ambazo hazikutajwa Serikali imedhamiria kuwa na mipango thabiti itakayotuwezesha kutatua changamoto mbalimbali za Vijana kama vile Afya, Elimu, Ukosefu wa Ajira, matumizi ya TEHAMA yasiyo sahihi, vijana kutopenda kufanya kazi, ukosefu wa maadili,utaifa, moyo wa kujitolea na uzalendo.
Awali mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu Duniani – UNFPA, Tausi Hassan amesema ni matarajio ya Serikali kuwa Sera mpya ya Maendeleo ya Vijana itakayoundwa itatoa dira ya miongozo kwa Wadau wote wa Maendeleo ya Vijana nchini ili kuwezesha kupanga na kutekeleza program mbalimbali zitakazopelekea kuwapo ustawi wa maendeleo ya vijana nchini.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Geita, Lilian Rwegoshora ambaye ni mmoja wa washiriki amewataka vijana waliohudhuria kutumia fursa adhimu waliyoipata kwenda kufikisha ujumbe katika maeneo yao kuhusu, fasiri ya kijana wa Kitanzania,uzalendo na utaifa, afya ya uzazi na afya kwa ujumla, namna ya kujitafutia ajira, hamasa katika elimu, umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(ICT) na ushirikishwaji wa vijana katika michakato ya maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, Mkurugenzi wa Utawala na Ujasiliamali Watu Bw.Peter Kalonga, amesisitiza kuwa maoni ya vijana yanahitajika kwa wakati huu ambao serikali inafanya kila jitihada ya kuwahudumia vijana na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli zenye kuleta maendeleo na kudumisha maadili ya Taifa letu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.