Mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kitaifa unatarajiwa kuanza hapo kesho tarehe 11 na kumalizika 12 septemba 2019, Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa iliyojiandaa vyema kuhakikisha mtihani huo unafanyika na kumalizika vizuri.
Akizungumza ofisini kwake Afisa elimu wa Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola amebainisha kuwa jumla ya shule 949 kutoka mkoa wa Mwanza zinatarajia kufanya mtihani huo ambapo katika idadi hiyo shule 850 ni za mfumo wa Kiswahili na shule 99 ni za mfumo wa kiingereza.
Aidha Ligola amebainisha idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani huo katika mkoa wa Mwanza wameandaliwa vizuri na wapo tayari kwa ajili ya mtihani huo hapo kesho.
“Mtihani huu unatarajiwa kufanywa na jumla ya idadi ya wanafunzi wapatao 68,078 ambao katika idadi hii wanafunzi 32,134 ni wavulana na 35,944 ni wasichana,” Alisema Ligola.
Ligola amebainisha kuwa idadi ya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona watakao fanya mtihani huu kutoka shule za mfumo wa kiingereza na mfumo wa Kiswahili nao pia wameandaliwa vizuri na wapo tayari kufanya mtihani huo kwani hakuna changamoto zitakazokwamisha kufanikisha kwa mtihani huo.
“Mtihani huu utahusisha wanafunzi wasioona 7 ikiwa wavulana ni 6 na msichana 1 pia wanafunzi 37 wenye uoni hafifu kutoka shule za mfumo wa kiswahili ikiwa wavulana 14 na wasichana 13 na upande wa shule za mfumo wa kiingereza ni wanafunzi 5 kati yao mvulana ni 1na wasichana 4,” Alisema Ligola.
Hata hivyo Ligola ameaisitiza kuwa vifaa vyote vya mtihani vimeshawasili na wanafunzi wote wako tayari kwa ajili ya kufanya mtihani huo.
“Tayari tumepokea vifaa vyote na hatuna upungufu wa aina yoyote kwa upande wa watahiniwa pamoja na wasimamizi,”
Awali Ligola alianza kwa kuwatakia kheri wanafunzi wote watakao fanya mtihani huo wa kuhitimu darasa la saba na kuwatia moyo kuwa watafanya vyema na kuleta heshima katika mkoa wa mwanza.
“Ninawatakia kila la kheri wanafunzi wote wa darasa la saba katika mtihani wenu wa kuhitimu elimu ya msingi na ninaimani mmejiandaa vyema katika mtihani wenu na ni matumaini yangu kuwa mtafaulu vizuri na kuleta heshima katika mkoa wetu,”
Pamoja na hayo Ligola amewaomba wazazi wa wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani wahakikishe wanafunzi hao wanafanya mtihani, pia ametoa onyo kwa wazazi wanaowashawishi watoto wao kufanya mtihani vibaya ili wasifaulu kuacha tabia hiyo, lakini pia amewataka wasimamizi kusimamia vizuri na kuacha udanganyifu katika mtihani ili kuweza kupata matokeo ya haki.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.