Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba,amewataka wakulima kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) ili kupata taarifa sahihi za kiwango cha mvua waweze kuchagua aina ya mazao watakayolima.
Tutuba ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza na wadau wa sekta ya kilimo Mkoa wa Mwanza, kutoka taasisi za Serikali na binafsi kwenye mkutano ulioandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza uliolenga kujadili changamoto zilizopo katika sekta hiyo ili kuboresha uzalishaji na masoko ya mazao ya biashara na chakula.
Alisema ukosefu wa taarifa sahihi za hali ya hewa ni miongoni mwa changamoto zinazosababisha wakulima kuvuna mazao kidogo kwa sababu wanalima mazao bila kujua kiwango cha mvua kitakachokuwepo mwaka husika wa kilimo.
” Serikali inaweka mazingira wezeshi kwa wakulima lengo ni kila mkulima afaidike na shughuli hiyo, lakini baadhi yao wanakosa taarifa sahihi za hali ya hewa kuna mazao hayahitaji mvua nyingi na mengine yanahitaji mvua chache.
“Ili mkulima aweze kuamua zao lipi alime kulingana na kiwango cha mvua kwa mwaka husika ni wajibu wetu sisi wadau wa sekta ya kilimo wote wa taasisi za Serikali na binafasi kuwafikishia taarifa hizo kutoka TMA,”alisema.
Alisema Mkoa wa Mwanza unazo fursa nyingi za kilimo ikiwemo mvua za kutosha na ardhi yenye rutuba pia ni kitovu cha masoko hivyo wakizitumia vizuri wakulima wengi watanufaika kwa kufanya kilimo biashara.
“Lazima tuwe wabunifu tuangalie ni changamoto gani zinazosababisha tija iwe ya chini, jukumu letu sisi wadau wa kilimo tuzibainishe, tuwaelekeza na kuwashawishi wakulima wetu wazingatie kanuni bora kilimo .
Aliwashauri wadau hao kuwafundisha wakulima kutunza takwimu za gharama walizozitumia katika kilimo ili wahakikishe wanalima mazao ambayo yatawaingizie kipato na si kuwapa hasara.
Miongoni wa mazao yatakayopewa kipaumbele katika Mkoa wa Mwanza ni pamoja na mahindi, pamba, mtama, alizeti, mpunga, muhogo, dengu mboga na matunda.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.