MWANZA YAADHIMISHA MIAKA 60 YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Mkoa wa Mwanza leo umeadhimisha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,huku yakielezwa mafanikio mbalimbali ndani ya Muungano huo ukiwemo mshikamano miongoni mwa Watanzania na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Akizungumza na wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye viwanja vya Furahisha,Katibu Tawala wa Mkoa huo,Ndg. Balandya Elikana amebainisha mshikamano wa Kitaifa tulionao umeondoa ubaguzi licha ya kuwepo na wingi wa makabila hapa nchini.
"Ndugu wananchi tuna kila sababu ya kuulinda na kuutetea Muungano wetu,mtu wa kutoka Bara anaweza kwenda Zanzibar na mtu wa kutoka visiwani humo ana uwezo wa kuja huku bila ya vikwazo vyovyote,hali hii ndiyo imelijenga Taifa imara la Tanzania.
Amesema waasisi wa Muungano huu Hayati Baba wa Taifa,Julius Nyerere na Abeid Aman Karume tuwaenzi kwa kuzidi kuimarisha Umoja wetu huku ukileta tija kwa kila upande.
"Miongoni mwa mafanikio ya Muungano wetu tunaona miradi mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi ikifanyika,hapa Mwanza tuna ujenzi wa Reli ya kisasa SGR,Daraja la JP Magufuli,Meli ya Mv Mwanza na upanuzi wa uwanja wa ndege,"Balandya.
Aidha ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia kwa kuzidi kuimarisha sekta za afya, elimu na kilimo tukiadhimisha miaka 60 ya Muungano tukiona sekta hizo zikizidi kuwa na tija kwa kuleta mageuzi ya kimaendeleo kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ambapo sherehe hizo Kimkoa zimefanyika wilayani humo,Katibu Tawala wa Wilaya hiyo,Wakili Mariam Msengi amebainisha wameadhimisha sherehe hizo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi sehemu kadhaa, kupanda miti na kufanya mashindano ya burudani.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umefanyika Aprili 26,1964 chini ya waasisi Hayati Julius Nyerere na Abeid Karume.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano inasema Tumeshikamana,Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.