Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka wazazi kutokuficha na kunyanyapa watu wenye ulemavu na kutoa angalizo kuwa kila mtoto ana kipaji chake.
Akizungumza leo februari 23, 2023 katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza ambapo maadhimisho hayo yamefanyika Kitaifa Mhe.Malima amesema Serikali ya awamu ya 6 chini ya Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa watu wenye ulemavu imezindua Mwongozo wa Taifa wa Utambuzi wa Mapema na Afua Stahiki kwa watoto wenye ulemavu wa mwaka 2021,pia Mwongozo wa Utekelezaji, Ujumuishwaji na Uimarishaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu wa mwaka 2022.
"Serikali kwa mwaka 2022,imeandikisha watoto 2,883 katika elimu ya swali ambapo wasichana 1,413 na wavulana 1,470, wakati Shule ya Msingi 3,318 na MEMKWA 122," amesema Mhe.Malima.
Hata hivyo amesisitiza kuwa Serikali imeajili Kada ya walimu nafasi 9800 na kada za afya 7612 ambapo jumla ya watu wenye ulemavu 261 sawa na asilimia 2.7 walikidhi vigezo na kupata ajira ya ualimu ambapo kati ya hao 261ya watu wasioona walikuwa 61.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Joy Maongezi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau imetoa Fimbo nyeupe 35, viti mwendo 35 na mafuta kinga 35 pamoja na miwani kwa wanafunzi 174, Essilor glasses 174,miwani yenye lenzi inayobadilika kulingana na mionzi ya jua 172, monocular 268, makasha ya miwani 183, mabegi 341 pamoja na viungo bandia kwa watu 179 vyenye thamani ya shilingi 118,552,000 kutoka Taasisi ya Lohana.
"Serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na masuala ya Elimu, uwezeshwaji wa kiuchumi, afya na ajira," amesema Bi. Maongezi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa maafisa Elimu wa Elimu maalumu Issa Kambi, amesema Maafisa Elimu wa Elimu maalum ndiyo kiini cha maandishi ya Braille na ameahidi kuendelea kujitoa kwa hali na mali katika kusimamia elimu kwa wanafunzi wasio na usoni.
Akisoma risala kwa niaba ya Wasioona kwa mgeni rasmi, Mshauri wa Jumuiya ya Maendeleo ya wasioona Tanzania James Shing'wenye amesema anashukuru Serikali kwa kuja na wazo la bima ya afya kwa wote kwani wengi wa wenye ulemavu hawana uwezo wa kugharamia matibabu hivyo bima ya afya ni ukombozi kwa wote.
"Tunaiomba serikali iweke mifumo mizuri ya Usalama katika miundombinu ya mashuleni na maeneo ambayo wasioona wanapatia huduma, walimu wa elimu maalum waongezwe pamoja na kupatiwa motisha," amesema Shing'wenye.
Aidha, ameiomba Serikali kuongeza vyuo vya walimu wa elimu maalum na motisha, pia iboreshe mazingira na mahitaji kwa wanafunzi wasioona pamoja na mashine za kidijitali za kuandikia.
Pamoja na hayo, Shing'wenye ameiomba serikali kutenga bajeti maalumu ya maadhimisho ya kila mwaka kwa ajili ya wasioona pamoja na kuanzisha mpango maalumu wa bima ya afya kwa watu wasioona.
Naye, Mwenyekiti wa chama cha wasioona Tanzania Omar Itambu amesema kwa hapa Tanzania 1960 maandishi ya Braille yalianzia Shule ya Msingi Buigiri huko Dodoma na imekuwa ni ukombozi mkubwa kwa wasioona kwani hata yeye mwenyekiti amesoma kupitia maandishi haya ya Braille.
"Niwaase wazazi wote ukipata mtoto mwenye ulemavu wowote ule, mpeleke Shule siku hizi hakuna kinachoshindikana,"amesema Itambu.
"Sasa hivi Serikali inatujali sana, japokuwa changamoto haziishii.....hivyo tunaiomba serikali kuingia kwenye mfumo wa dijito Braille ambao utapunguza ama kumaliza changamoto za wasioona," amesisitiza.
Siku ya Kimataifa ya maandishi ya Braille huadhimishwa kote duniani tarehe 4 Januari ya kila mwaka, kwa mwaka huu yamebeba Kauli mbiu ya "Eneza Ufahamu Kuhusu Umuhimu wa Braille."
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.