Sekta ya Elimu Mkoa wa Mwanza imesema itaendelea kutoa haki sawa kwa jinsia zote katika kuhakikisha kila mtu mkoani humo anapata elimu bora ikiwa ni katika kuhakikisha kila mwananchi anapata silaha hiyo adhimu kwenye maisha.
Hayo yamebainishwa leo na Afisa Tarafa wilaya ya Sengerema Bi. Happiness Segere alipozungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima sherehe zilizofanyika kwenye viwanja vya Jeshi Wilayani Sengerema.
Bi. Segere amesema ni lazima jamii itambue umuhimu wa elimu na amefafanua kuwa Watu wazima wanaoelimisha watoto wao wanaendelea kujijengea uwezo mkubwa wa kusimamia Elimu ya watoto wao tofauti na wale wasiojielimisha.
"Ni jukumu letu sote kuhamasisha watu mbalimbali kujiunga na mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa na vilevile walioikosa ya Sekondari na programu zingine ili waweze kujielimisha juu ya shuguli wanazofanya na kuweza kujua kusoma, kuandika na kuhesabu." Amesema Bi. Segere.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa, Mwalimu Nyangi Msemakweli amesema Mkoa wa Mwanza una jumla ya wanafunzi 4222 walio chini ya mfumo usio rasmi ambao wanahudumiwa na walimu 115 kwenye Vituo, Shule za Msingi na Vituo vya Elimu ya watu wazima na kwamba kuna vituo mbalimbali vya Ufundi stadi vinavyosaidia vijana kuwezeshwa kiuchumi.
Bi. Ritha Rafael, Kaimu Mkufunzi Mkazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Mkoa ametoa wito kwa Mabinti waliokatisha Elimu ya Sekondari kwa sababu mbalimbali kujiunga na Mfumo wa Elimu ya Watu Wazima kwenye vituo 14 vilivyo kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo ili wapate Elimu ya Sekondari kwa muda mfupi na kutimiza ndoto zao.
"Mwanzoni watu wazima walikusanyika chini ya miti na kujifunza kusoma lakini sasahv maendeleo ni makubwa kwani watu hawa wanapata nafasi ya kuendelezwa pia kwenye stadi za maisha kwa kujifunza kusoma na kufanya shughuli za kiuchumi nje ya Elimu isiyo rasmi." Amesema Mwalimu Rafael.
"Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema ni moja ya vyuo 54 nchini ambavyo asili yake ni funzo alilolioata Mwalimu Nyerere nchini Sweden miaka ya 1960 ambapo alikuta mfumo wa vyuo vya maendeleo ambavyo wananchi wanapata stadi za kazi katika fani mbalimbali kama Umeme, Uashi, kilimo, ufugaji na uchomeleaji Chuma kutokana na mahitaji nje ya mfumo rasmi na ndipo mwaka 1978 akavianzisha hapa nchini." Mkuu wa Chuo, Hagai Shilah.
Maadhimisho hayo adhimu ya Juma la Elimu ya Watu wazima ngazi ya Mkoa yalianzia kwa Maafisa kutembelea vikundi 18 vya wajasiliamali waliowezeshwa chini ya mpango wa Elimu nje ya mfumo rasmi ambavyo vinavyojihusisha Kilimo, Uvuvi, Uashi na Ufugaji na kubaini changamoto kama za Mtaji, Pembejeo na Masoko ambapo waliwapatia Elimu ya kukabiliana nazo.
Timu ya Walimu imewapongeza vikundi vya Tuungane na Amkeni kwenye kijiji cha Katunguru imeahidi kufikisha changamoto hizo kwenye mamlaka husika kwenye Halmashauri ambako wataweza kusaidiwa kupata mikopo kupitia vikundi vya akina mama na pia uwezekano wa kupata soko la bidhaa kwenye Shule za Sekondari na kupata mgao wa mbolea za ruzuku.
Vilevile, timu hiyo ilifika kwenye kituo Cha Elimu Sengerema kinachowafua watoto nje ya mfumo rasmi na kuweza kufikia malengo yao ambapo pamoja na mafanikio makubwa ya ufaulu kwenye kituo hicho wana tatizo la mafunzo ya vitendo kwenye Masomo ya Sayansi ambapo wameiomba Serikali kuwapatia uwezo kwenye eneo hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.