Mkoa wa Mwanza unakabiliwa na upungufu mkubwa wa miundombinu ya elimu, hali inayoufanya uongozi wa mkoa kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na upungufu huo.
Hayo yameelezwa jijini hapa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza Mwl. Michael Ligola alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya elimu mkoa kwenye mkutano wa wadau wa elimu, kikao ambacho kilihudhuriwa pia na Wakuu wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi watendaji kwa wilaya zote za mkoa.
Alisema kwa upande wa shule za msingi, Ligola alisema mkoa unakabiliwa na upungufu wa walimu 4,878 kati ya walimu waliopo 12,684 na kwa upande wa shule za sekondari zinahitaji jumla ya walimu 4,332 kwa masomo ya Sanaa na waliopo ni 4,077 na upungufu ni walimu kwa 389 katika halmashauri za Sengerema, Manispaa ya Ilemela na Magu.
“Kwa upande wa walimu wa sayansi, tuna upungufu wa walimu 1,765 kwa halmashauri zote na waliopo ni 1,351 na mahitaji ni walimu 3, 116,” alisema.
Kwa upande wa vyumba vya madarasa, Ligola alisema mkoa una upungufu wa vyumba vya madarasa 10,411, matundu ya vyoo 23,485 na nyumba za walimu 14,842
“ Kwa upande wa sekondari tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 1,513, matundu ya vyoo 4,525, maabara 137 na nyumba za walimu 4,586,” alisema.
Aidha Ligola alisema kumekuwepo na mdondoko wa wanafunzi kwa ngazi mbalimbali za elimu kimkoa, ambapo kwa mwaka huu jumla ya wanafunzi 16,780 sawa na asilimia 19.8 ya walioandikishwa darasa darasa la kwanza mwaka 2013 hawakuhitimu elimu ya msingi.
“Sababu iliyosababisha mdondoko huo ni utoro unaosababishwa na umbali kufika shuleni, migogoro ya ndoa, utovu wa nidhamu, ajira za utotoni, ukosefu wa hosteli na mimba,” alifafanua.
Aliwataka wadau wa elimu kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuchangia miundombinu ya elimu kwa madai kuwa serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake.
Kwa upande wao, wakuu wa wilaya zote wa mkoa wa Mwanza, ambao kila mmoja alikuwa akivutia upande wake, walisema watahakikisha wanaweka mikakati imara itakayosaidia kuongeza viwango vya ufaulu ili kuuwezesha mkoa wa Mwanza kuwa wa kwanza kitaifa.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Colnel Maghembe ambaye wilaya yake nafasi ya 115 kitaifa kutoka nafasi ya 130 mwaka jana na nafasi ya 4 kimkoa kutoka nafasi ya 8 kimkoa kwa mwaka jana, alisema siri ya mafanikio ya ushindi huo ni kujenga mazingira mazuri kwa walimu kwa kushirikisha jamii, wanafunzi na walimu.
Akiahirisha mkutano huo wa wadau wa elimu, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela aliwataka viongozi wote wa wilaya kutobweteka na ushindi waliopata kwa mwaka, bali wawe na mipango kazi inayotekelezeka katika suala zima la elimu.
“Wakuu wa wilaya nendeni mkatatue changamoto za elimu kwenye maeneo na fundisheni vijana wetu uzalendo,” alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.