MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MRADI WA MAJI YA BOMBA WA BILIONI 2.9 CHIFUNFU-SENGEREMA
Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye mradi mkubwa wa maji ya bomba katika kata ya Chifunfu-Sengerema unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) kwa zaidi ya Bilioni 2.9 kutoka chanzo cha mfuko wa maji wa Taifa (NWT).
Akizungumza kwenye hafla hiyo leo Julai 17, 2023, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Abdalla Shaib Kaim amewapongeza Mkuu wa Wilaya, RUWASA na watendaji wa Sengerema kwa ujumla kwa usimamizi mzuri ulioleta matokeo ya mradi bora unaoendana na thamani ya fedha zilizotumika.
"Mwenge wa Uhuru 2023 umekagua mradi huu kwa kina na itoshe tu kusema ubora umezingatiwa na hakika RUWASA mmeonesha nia ya kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kumtua mama ndoo kichwani na kuwaletea huduma bora ya maji wananchi." amesema Ndugu Kaim.
Aidha, Ndugu Kaim ametoa wito kwa wakala huyo wa maji wa serikali kushirikiana na wananchi kuhakikisha wanapanda miti kwenye vyanzo vya maji na katika maeneo yote yanayozunguka miradi yao ili kuendelea kulinda na kuhifadhi vyanzo hivyo kwa vizazi vya sasa na baadaye.
Mhandisi George Genes Massawe
Meneja RUWASA Wilaya Sengerema amesema mradi huo mkubwa wa maji utainua hali ya upatikanaji maji safi na salama kwa wananchi 35343 kutoka vijiji vya Chifunfu, Nyakahako na Lukumbi kaya ya Chifunfu kutoka asilimia 6 hadi asilimia 88.9.
Mhandisi Massawe ameongeza kuwa mradi huo wenye vituo vya kuchotea maji 12 na tangi la ujazo wa lita laki 5 za maji utasaidia kupunguza magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama kama kichocho, kuhara, tumbo, amiba na mengineyo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu (CCM) amebainisha kuwa Serikali imetekeleza mradi huo ikiwa ni katika adhma ya Serikali ya kuwaletea huduma safi za maji kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilivyojibainisha wakati wa kampeni za Mwaka 2020 na kwamba haitaishia hapo bali wananchi hao wajiandae na mradi mkubwa wa barabara ili kuwapunguzia adha.
Vilevile, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye shule ya Sekondari Ibondo na kuagiza madirisha na madawati yarekebishwe kutokana na kutengenezwa kwa gharama za wahandisi na mafundi kwani wametumia mbao mbichi na mkandarasi alipe kodi ya zuio kiasi cha Milioni 1.8
Mkopo wa Tshs. Milioni 8 walizokopeshwa Kikundi cha vijana wanaojihusisha na utengenezaji wa Samani katika mtaa wa Ibisabageni zimetosha kuwainua kiuchumi kwani wanazalisha na kuuza bidhaa hizo hata kufikia hatua ya Mwenge wa Uhuru kuwatembelea kabla ya kuzindua kituo cha mafuta 'Kwa Neema' kilichogharimu zaidi ya Milioni 400.
"Fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri Kiasi cha Shilingi Milioni 50 zimejenga madarasa mawili na kutengeneza madawati 40 ambapo zitasaidia kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani na kuongeza kiwango cha ufaulu" amesema mwalimu Sundi Mussa wa Pambalu Shule ya msingi kwa niaba ya Mkurugenzi Sengerema wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Jengo la Wagonjwa wa Dharula linalojengwa kwenye Hospitali ya Wilaya hiyo kwa Shilingi Milioni 300 kutoka chanzo cha Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Udhibiti wa Ugonjwa wa Uviko 19 limewekewa jiwe la Msingi na Mkimbiza Mwenge ametoa wito kukamilishwa kwa haraka lakini kwa ubora unaotakiwa ili wananchi kutoka Kata 26 za Halmashauri hiyo na Halmashauri za jirani waweze kunufaika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.