Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia Vijana wa Mwanza wanaojishughulisha na Miradi ya Ufugaji wa Samaki kwa njia ya Vizimba kupata fedha Tshs Bilioni 2.5 walizoomba kama mkopo kutoka Benki ya Kilimo.
Ametoa wito huo leo Agosti 19, 2022 wakati akizungumza na Vijana wanayojihusisha na Miradi hiyo na amemuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa huo kufika Dodoma akiwa na vielelezo vya andiko la mkopo huo ili akutane na Wataalamu wa Wizara yake ili kukamilisha kupatikana fedha hizo.
"Natambua ugumu wa Benki kutoa fedha hizo lakini sasa nitatumia njia nyingine kwa kumuhusisha Waziri wa Mifugo na Wataalamu wengine kufanikisha kupatikana fedha hizo mwezi wa tisa" amesisitiza Naibu Waziri.
Amesema amevutiwa na utaratibu uliowekwa na Mkoa katika kufanikisha Miradi ya Ufugaji wa samaki kuwa bora kwa njia ya Vizimba kwa baadhi ya Vikundi vilivyopo Wilaya nne alizotembelea za Sengerema, Ukerewe, Ilemela na Nyamagana.
"Nimesikia kikundi cha Ufugaji samaki cha Ilemela walikwenda Uganda kwa ziara ya mafunzo, hii ndiyo njia sahihi ya kuongeza tija katika Miradi hii," amesema Mhe. Ulega.
Awali akizungumzia hali ya uzalishaji Mali Kwa Makundi ya Vijana Mkoani Mwanza, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na uzalishaji Emil Kasagara amesema Ufugaji wa Samaki kwa njia ya Vizimba umekuwa na faida kutokana na Vijana wengi kufaidika na kuondokana na kukaa vijiweni kwa kukosa ajira.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amebainisha wamejipanga kuhakikisha wanatimiza ndoto za Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kuona uchumi wa bluu unawanufaisha Vijana na makundi mengine.
Amezitaka Taasisi zote za fedha za Serikali na mamlala zingine za utoaji vibali kuacha kuwawekea vikwazo visivyo vya lazima wanaofika kwa mahitaji ya Miradi yao.
Naye, Mbunge wa viti Maalum Vijana Mkoa wa Mwanza Mhe. Ng'wasi Kamani amesema rasilimali ya Maji ya Ziwa Victoria itazidi kuwanufaisha hasa Makundi ya Vijana na kuiomba Serikali kuzidi kuwaongezea kiwango cha Mikopo ya fedha.
Naibu Waziri Ulega amekuwa na ziara ya siku nne Mkoani Mwanza kukagua Miundombinu iliyo chini ya Wizara yake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.