TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka Vyama vya Siasa nchini kufahamu majukumu ya tume hiyo badala ya kulalamika vinaonewa kutokana na mikutano ya hadhara kuzuiwa.
Pia imesema uboreshaji wa kipindi hiki hautahusisha wapiga kura wote waliojiandikisha mwaka 2015 bali wapya wenye umri wa miaka 18 na watakaofikisha umri huo siku ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020,waliohama kwenye maeneo yao ya awali ya uchaguzi, wenye kadi zilizoharibika ama kupotea na kuwataka kujiandikisha vituoni na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi wakiwemo waandishi wa habari, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Jiji la Mwanza.
Alisema vyama vya siasa ni wadau wakubwa wa uchaguzi lakini vinakabiliwa na changamoto ya kuchanganya majukumu ya NEC na ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambapo Tume inazingatia Katiba.
Jaji Mbarouk alieleza kuwa NEC mbali na Katiba, inafuata na kutekeleza matakwa ya kisheria, ambayo ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa na kanuni pamoja na sheria ya maadili ambayo vyama vyote visaini na kuweka masharti kwa kuzingatia maadili na taratibu za uchaguzi .
“Majukumu ya Tume ya Uchaguzi yameaninishwa kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 76 ambayo ni kusimamia na kuratibu mikutano ya kampeni kwenye uchaguzi wa Rais na wabunge.Malalamiko ya vyama vya siasa kuhusu katazo la mikutano ya hadhara si la NEC,”alisema Jaji Mbarouk.
Makamu mwenyekiti huyo wa NEC alitoa ufafanuzi huo kutokana na wadau wa uchaguzi Shaaban Itutu (ADC), Edward Mboje (CUF) na Katibu wa NLD Mkoa wa Mwanza, Bonaventura Ndekeja kudai kuwa Tume ya Uchaguzi imekaaa kimya ilhali demokrasia ikifinyangwa.
Akizungumzia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, Jaji Mbarouk alisema mafanikio ya zoezi hilo yanategemea ushiriki wa wadau wa uchaguzi huo wakiwemo Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Asasi za Kiraia, Wawakilishi wa makundi maalum na waandishi wa habari, ili kuleta mabadiliko chanya na mwamko wa maendeleo kwenye jamii.
“Nchi iko kwenye maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo NEC imepewa mamlaka ya kutekeleza majukumu ya msingi ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura.Sheria ya uchaguzi ya Serikali za Mitaa, NEC inapasa kuboresha Daftari la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine unaofuata,”alisema Jaji Mbarouk na kuongeza;
“NEC inawaarifu kuwa imeanza kuboresha daftari hilo baada ya kukamilika kwa maandalizi muhimu ya kuhakiki vituo vya kujiandikisha,uandikishaji wa majaribio, maandalizi ya vifaa vya uboreshaji daftari na mkakati wa utoaji elimu kwa mpiga.Tulianzia uboreshaji wa daftari hilo mkoani Arusha na Kilimanjaro Julai 18,2019 na utaendelea kwenye mikoa mingine kulingana na ratiba.”
Alisema kazi kubwa ya kupambana na mila potofu katika jamii zinazozuia ushiriki wa baadhi ya makundi ya watu wenye ulemavu na wanawake kwenye shughuli za kimaendeleo, kijamii na kisiasa (chaguzi) imepata mchango mkubwa.
Makamu mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi alieleza kuwa Mkoa wa Mwanza wenye vituo 2,178 kutoka vituo 2,117 vya awali, uboreshaji daftari hilo la kudumu utaanza Agosti 13 hadi 19, mwaka huu kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (BVR) utakaochukua na kutunza taarifa za mpiga kura ambao pia umehakikiwa.
Aliongeza kuwa uhakiki wa vituo ulifanyika kuona kama bado vina hadhi ya kuendelea kuwa vituo vya kuandikisha wapiga kura na ulilenga kuona iwapo kuna maeneo ya kuongeza vituo kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Pia Asasi za Kiraia 24 kati ya 52 zimepewa vibali vya kutoa elimu kwa wapiga kura kwenye maeneo mbalimbali na kuzitaka kutumia mwongozo wa utoaji elimu hiyo utakaohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu uliotolewa na Tume ambapo pia vyombo vya habari vitatumika kufikisha elimu hiyokwa jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.