Mashirika yasiyo ya Serikali (NGOS) na asasi za kiraia zilizopata usajili kutoka Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA) na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) yameanza kusajiliwa upya.
Mashirika hayo hivi sasa yatasajiliwa chini ya msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali iliyopo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ambapo tayari usajili huo unaanza leo mkoani Mwanza hadi Agosti 13, mwaka huu.
Akizungumuza na waandishi wa habari jijini Mwanza, Msemaji wa wizara hiyo ,Idara ya Maendeleo, Erasto Ching’oro alisema zoezi hilo linafanyika kulingana na sheria ya mashirika yasiyo ya Serikali.
“Usajili huu unafanyika kutekeleza matakwa ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) iliyofanyiwa mabadiliko yanayolazimu mashirika ya kijamii ambayo awali yalisajiliwa chini ya sheria nyingine kama Brela na Rita na sheria ya asasi za kijamii kujisajili upya katika ofisi ya msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali iliyopo wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto.
“Pia usajili huu unahusisha mashirika mapya ambayo kwa mara ya kwanza yanaomba kusajiliwa lakini nitoe angalizo kuwa waliosajiliwa chini ya sheria ya NGOs namba 24/2002 na wale waliopewa cheti cha certificate of compliance kwa sasa zoezi hili haliwahusu ila wao watapewa maelekezo baadaye.
“Huduma ya usajili itafanyika bure kabisa hivyo niwaombe wote ambao zoezi hili linawahusu kuzingatia muda na kuachana na dhana iliyozoeleka ya wananchi wengi kusubiri siku za mwisho ndipo wanafurika japo tutaongeza muda kama tutalazimika kufanya hivyo,”alisema Ching’oro.
Ching’oro alisema jamiii inapaswa kufahamu kuwa mbali na kutekeleza matakwa ya mabadiliko ya kisheria lakini pia zoezi hilo limelenga kuimarisha utawala bora, uwazi, uwajibikaji wa mashirika, kuimarisha utaratibu katika ngazi zote, kutambua mchango wa NGOs pamoja na kuhakikisha kuwa utaratibu unakuwa na maslahi mapana ya kitaifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.