NI LAZIMA TUIHESHIMU NA KUITHAMANI AMANI TULIYONAYO - RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa Wananchi na wakazi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kuitunza, kuthamini na kuiheshimu amani iliyopo kwa kuwa ndio tunu ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo Machi 20, 2025 wakati wa hafla ya iftari iliyoandaliwa na Tawi la Benki kuu ya Tanzania Mwanza ambapo amesema Amani ya Nchi yetu ndio msingi wa mafanikio tuliyonayo na tunayoyatarajia
Kadhalika Mhe. Mtanda ameendelea kwa kusema amani hiyo pia inachochewa na uwepo wa Viongozi imara na madhubuti wakiongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo kama Taifa hatuna budi kumuombea kila wakati ili Taifa liendelee kuwa na utulivu.
“Hata vitabu Vitakatifu vinatuambia kuwa tuheshimu mamlaka kwa maana mamlaka zote zinatokea juu, hivyo hatuna budi kumuheshimu na kumuombea Rais wetu”.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amewapongeza Tawi la benki kuu Mwanza kwa kuwakumbuka Yatima, wenye mahitaji maalum na Wajane na kuwapa zawadi mbalimbali zitakazowasaidia katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na Kwaresma.
Naye Mkurugenzi wa Tawi la Benki Kuu Tanzania Mwanza, Bi Gloria Mwaikambo amesema wataendelea kuimarisha uhusiano baina ya benki na wadau wao.
Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhajj Hassan kabeke amewataka waislamu waliohudhuria iftari hiyo kuendelea kutenda matendo mema na kuachana na vitendo vya uvunjifu wa amani hususani katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.