RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMALIZA KERO YA MAJI MWANZA : RC MAKALLA
*Ampongeza Rais Samia kutoa fedha Bilioni 70 upanuzi chanzo cha maji Butimba*
*Ametoa fedha kupanua Chanzo cha maji Capripoint*
*Aelekeza ujenzi wa Matanki 5 makubwa uanze*
*Atinga Site kukagua ukarabati wa bomba lililoharibiwa na mvua Kishiri*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa chanzo cha maji Butimba uliokamilika Oktoba 30, 2023 ukijengwa kwa zaidi ya Bilioni 70 na kuzalisha Lita Milioni 48 kwa siku na akatumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo.
Akizungumza leo kwenye chanzo cha mradi huo kilichopo kwenye kata ya Butimba Makalla amesema Mhe. Rais ameamua kwa dhati kumtua Mama ndoo kichwani kwa kumuondolea adha ya upatikanaji maji mkoani humo jambo ambalo awali lilikua ni kama ndoto kulifikia.
"Leo ni mara ya nne nimefika hapa ikiwa ni katika kusukuma ili mradi ukamilike, nawapongeza wote kuanzia Mkandarasi na viongozi kwa kutekeleza mradi huu ambao ni wa kisasa kabisa kwa jinsi mitambo niliyoiona ikifanya kazi, nachotaka sasa tuongeze nguvu kwenye ujenzi wa matanki na usambazaji," amesema Makalla.
Katika kuhitimisha ziara yake kwenye miradi ya maji Mwanza, Mkuu wa Mkoa amefika kweye mtaa wa Kishiri Bushitu kukagua ukarabati wa bomba lililoharibiwa na mvua na ameahidi kurekebisha hali hiyo mapema iwezekanavyo na akabainisha kuwa wananchi wa eneo hilo wanatarajiwa kujengewa barabara kwa kiwango cha lami KM 22 kutoka Buhongwa siku za usoni
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Nelly Msuya amebainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha si tu wananchi waliotajwa kwenye usanifu bali hata wengine nje ya mradi kwa kushirikiana na usambazaji wa maji yatokayo kwenye chanzo cha Capripoint.
Awali Mhandisi Selestine Mahubi ambaye ni Msimamizi wa mradi huo alifafanua kuwa wananchi wa mitaa ya Igoma, Kishiri, Ndose, Nyamaliwa, Nyamhongolo, Kisesa, Kanyama, Malimbe na Luchelele wananufaika na kwa upanuzi wa awamu ya pili watanufaika Usagara, Fela, Bukumbi, Nyashishi na Misungwi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.