RAIS SAMIA AZINDUA UGAWAJI WA VIZIMBA VYA KUFUGIA SAMAKI NA BOTI ZA KISASA MWANZA
*Ameipongeza Wizara kwa mradi huo kwa kushirikiana na TADB*
*Amewataka wanufaika kuwa waaminifu kwa kufanya marejesho ya Mkopo*
*Asema Serikali imejipanga kuboresha sekta ya Uvuvi nchini*
*Aagiza ujenzi wa Miundombinu ya kuhifadhi Samaki Uwanja wa ndege Mwanza*
*Awataka wavuvi kufuata Sheria na Wizara kusimamia nyavu zinazokubalika*
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Januari 30, 2024 amezindua Ugawaji wa Vizimba vya Kufugia Samaki 222 kwa wanufaika 1213 na Boti za Kisasa 55 kwa Wavuvi ywa Kanda ya ziwa 989 vyenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2.
Akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Nyamagana Mhe. Rais amesema Serikali itaendelea kuinua Sekta ya Uvuvi kwa kuweka vipaumbele kwenye bajeti na juhudi za kukuza Sekta na kwamba ipo tayari kupokea mapendekezo ya kuinua sekta hiyo kadiri inavyowezekana.
"Kwa muda mrefu Sekta hii ilikua kwenye Sekta binafsi ila kuanzia sasa tumeamua kuweka mfumo rasmi wa kurasimisha wavuvi, wakuzaji wa viumbe maji na wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo ili kwa makusudi tuweze kuinua sekta hii kwa maendeleo ya uchumi wa buluu." Rais Samia.
Aidha, Mhe. Rais amewataka wavuvi kufuata Sheria za Uvuvi na Wizara kutoa elimu ya madhara ya uvuvi haramu na kusimamia kwa ukaribu Nyavu zinazokubalika ili kutokomeza uvuvi haramu nchini kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadae.
Akijibu risala ya wanufaika Rais Samia ametoa Rai kwao kufanya vizuri kupitia mradi huo ili sekta binafsi ziweze kuvutwa kama mabenki ili wadau kwenye sekta hiyo waongezeke kutokana na upatikanaji wa mitaji kupitia mikopo nafuu, na amewataka wanufaika kuwa waaminifu kwa kurejesha fedha za mkopo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdalah Ulega amemshukuru Rais Samia kwa kutoa jumla ya Bilioni kwa 60 2022/23- 2023/24 kuendeleza mialo, mashamba darasa ya Ufugaji na kwa mwaka 2024/25 wamejipanga kuwasaidia zaidi wananchi kuinuka kiuchumi kwa kuwa na boti za kisasa 500.
"Sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta yenye mchango mkubwa wa ukuzaji uchumi wa nchi, sekta hii imezalisha zaidi ya ajira milioni 4.5 zinazojumisha wavuvi wa asili na wakuzaji na wakulima wa mwani na kusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye usalama wa chakula." Mhe. Ulega.
Katibu Mkuu wa CCM Taifa. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametumia wasaa huo kumsifu Rais Samia kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama ya 2020- 25 hususani sekta ya Uchukuzi na Ujenzi huku akitolea mfano wa Uboreshaji wa barabara nchini kwa kujengwa kiwango cha lami na kuunganisha Mikoa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Frank Nyabundege ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuiwezesha Benki hiyo kwa turufu kwani imeanzishwa 2015 ikiwa na mtaji wa Bilioni 60 tu lakini ndani ya uongozi wake ametoa Bilioni 208 kwa wakati mmoja na ameahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuwezesha wavuvi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amebainisha kuwepo kwa Uvuvi haramu na kwamba mkoa umeshachukua hatua kwa kutoa maelekezo 11 kwenye Mkutano wake na Wadau wa Sekta hiyo katika kuhakikisha unakomeshwa na kuwa na uvuvi endelevu kwa ukuzaji wa uchumi wa buluu.
"Tunakushukuru sana Mhe. Rais kwa kutuzindulia Vizimba 222 na na Boti za Kisasa 55, tunaendelea kutoa Elimu ya ufugaji wa kutumia vizimba ili kukomesha uvuvi haramu na kuhakikisha tunawatunza Samaki walio ziwani ili waendelee kuongezeka." Makalla.
Naye, Pius Mtenya mnufaika wa Mradi wa Boti na Vizimba pamoja na vifaranga na chakula cha samaki ametumia wasaa huo kutoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuwapatia zana hizo ambazo zitasaidia kuwainua kiuchumi na akatumia wasaa huo kuomba uboreshaji zaidi wa miundombinu ya Sekta hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.