RAS BALANDYA ATAKA AFUA ZAIDI ULINZI NA USALAMA KWA WATOTO WA KIUME KAMA ILIVYO KWA WA KIKE
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amewasihi watumishi na wadau wa afya mkoani humo kuhamasisha na kuongeza jitihada za kulinda watoto wa kiume dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuongeza zaidi afua zinazolenga kundi hilo kama ilivyo kwa watoto wa kike.
Amesema hayo Julai 11, 2024 alipotembelewa na timu inayofanya ufuatiliaji wa afua za mradi wa DREAMS unaotekelezwa katika kata 18 kwa wanafunzi waliopo shuleni (shule za msingi 73) unaolenga kusaidia binti balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka (15 – 24) wasiosoma (out of school) wilayani Nyamagana.
"Ni furaha yangu kubwa kuona timu inayofanya ufuatiliaji wa ubora wa takwimu za mradi wa DREAMS unaotekelezwa na Serikali pamoja na wadau wetu ICAP na ELCT/ KKKT wilayani Nyamagana, takwimu zinapokua sahihi na zenye ubora ndipo tunaweza kupanga mipango yenye tija ya kutatua changamoto zilizopo.
Aidha, Katibu Tawala Balandya amesisitiza kufanya usimamizi shirikishi mara kwa mara kwa walengwa ili kufuatilia maendeleo yao na kutatua changamoto zao na kuhakikisha ustawi bora wa jamii.
Aidha, ametumia wasaa huo kutoa ombi kwa wadau hao kwa wakati mwingine kuona namna ya kuwahusisha watoto wa kiume waliopo shuleni na nje ya mifumo rasmi ya elimu ili nao waweze kunufaika na programu za DREAMS kwani nao wapo kwenye hatari ya maambukizi hayo hususani nyakati hizi za wimbi kubwa la ukatili wa kijinsia.
Ameongeza kuwa mradi huo umelenga kuwaibua mabinti zaidi 13,000 ndani ya mwaka wa mradi (OCT 23-SEP 24) kutoa huduma ya upimaji na ushauri nasaha kwa mabinti kutambua sehemu salama ambazo mabinti wanajifunza masomo na uendeshaji wa vipindi na elimu mbalimbali za kujiinua kiuchumi.
"DREAMS (in school) - Inayotekelezwa na mdau wetu- KKKT kupitia mradi wa USAID kizazi hodari kanda ya kaskazini mashariki imeweza kuwafikia mabinti 11,546 (99%) katika lengo la mwaka (FY2024 ) kufikia mabinti 11,572 katika shule 73 ambazo ziko katika mpango huo ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Nyamagana." Amefafanua Bw. Balandya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.