RAS BALANDYA ATANGAZA MATOKEO YA DARASASA LA SABA KANDA YA ZIWA, MWANZA YANG'ARA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana leo Juni 13, 2024 ametangaza matokeo ya Mtihani wa Utamilifu kwa darasa la Saba Kanda ya ziwa huku Mwanza ikiing'ara kwa ufaulu wa asilimia 84.6 kwa jumla ya wanafunzi 219,655 waliofanya mtihani huo.
Akitangaza matokeo hayo kwa niaba ya Makatibu Tawala wa Mikoa 5 ya Kanda ya ziwa, Elikana amebainisha kuwa nafasi ya pili imekwenda Mkoa wa Simiyu waliopata ufaulu wa 81% ikifuatiwa na Geita wenye ufaulu wa 72.6%,wakati Kagera wakiwa nafasi ya nne ya ufaulu wa 62.4% na Mara wakiwa na 52.8%.
"Rai yangu kwenu Maafisa Elimu mliohudhuria hafla hii tuzidi kuongeza bidii kwani takwimu zinaonesha masomo matatu ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi na Teknolojia wanafunzi hawajafanya vizuri, tulibebe jukumu hili kabla ya wanafunzi hawajafanya mtihani wao wa kumaliza elimu ya msingi Septemba mwaka huu", amesisitiza Balandya.
"Tunapaswa kuiunga mkono Serikali ya Rais Samia ambayo imeleta zaidi ya Tshs. bilioni 16 kwa mikoa ya Kanda ya ziwa (2023/24) Mwanza ikipata shs bilioni 4.3 kwa ajili ya kuboresha elimu ukiwemo ujenzi wa shule mpya, nyumba za walimu na matundu ya vyoo," Balandya.
Akitoa taarifa fupi ya mtihani huo wa Utamilifu kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Afisa Taaluma Mkoa anayeshughulikia elimu ya Sekondari Aisa Rupia amesema mtihani huo umefanyika Mei 22 hadi 23 mwaka huu ikijumuisha Halmashauri 37 yenye jumla ya shule 4205 kati ya hizo 3834 za Serikali na 371 za binafsi.
"Ndugu Mwenyekiti watahiniwa wamepimwa katika masomo sita ambayo yanafundishwa kulingana na mtaala mpya ulioboreshwa ambayo ni Hisabati, Kiingereza,Kiswahili,Sayansi na Teknolojia,Maarifa ya Jamii na stadi za kazi, na Uraia na Maadili,"Rupia
Wakati huo huo Elikana, leo asubuhi Ofisini kwake amekutana na uongozi wa Shirika linalowasaidia watoto wa kike elimu ya stadi za maisha kuanzia kidato cha kwanza, CAMFED TANZANIA ambao watafanya shughuli hiyo kwenye wilaya za Magu, Misungwi, Kwimba na Halmashauri ya Buchosa.
Katika mazungumzo mafupi mtendaji huyo wa Mkoa ameutaka ujumbe huo ambao ni walimu kitaaluma kuweka mkazo wanafunzi kuyapenda na kuyachangamkia masomo ya Hisabati na Sayansi.
Kiongozi wa kundi hilo Mussa Siame amesema mwaka huu wamepangiwa maeneo hayo na changamoto watakazo zibaini wataziwasilisha Tamisemi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.