Wadau wa Vyama vya Ushirika wanaoendelea kupata mafunzo maalum ya kutoka Analogia na kuingia Kidigitali wamepewa rai elimu hiyo ikalete mageuzi chanya kwenye vituo vyao vya kazi.
Akifungua Mafunzo hayo leo Jijini Mwanza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana, Katibu Tawala msaidizi Uchumi na Uzalishaji Ndugu Emil Kasagara amebainisha kumekuwa na upotezu wa nyaraka na kazi kuzorota kutokana na kutumia utaratibu uliopitwa na wakati ambao umechangia kurudisha nyuma kasi ya maendeleo kwenye Vyama vya Ushirika.
"Ndugu zangu mliopo hapa kwa haya mafunzo msione aibu katika kujifunza siku zote tatu mtakazo kuwa hapa, mkumbuke kuelimika kwenu kunakwenda kuleta taswira mpya katika majukumu yenu ya kila siku kwenye vituo vyenu vya kazi." Amesema Kasagara.
Kasagara amebainisha kuwepo kwa hati chafu na migogoro isiyokwisha, kutokuwepo kwa uwazi wa uwajibikaji kwenye Vyama vya Ushirika na kwamba muarobaini wake ni matumizi ya TEHAMA katika rahisisha utoaji huduma bora kwa Wananchi.
Mrajisi Msaidizi kutoka Mkoa wa Mara, Kija Maheda amesema baadhi ya Viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza vyama hivyo lakini hawakuwa na nia njema wametumia udhaifu huo wa mfumo duni kujinufaisha, lakini sasa kwa hatua hii mpya wanaoingia na jinsi Serikali hii ya awamu ya Sita ilivyonuia kuviinua Vyama vya Ushirika watasimama imara kuleta tija ya Maendeleo.
"Vyama vya Ushirika vinachangia ukuaji wa Uchumi wa Taifa letu, na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima ametuahidi kutupigania kuwa na Benki yetu ya Taifa ya Ushirika hivyo tuna kila sababu sisi Viongozi kuwa chachu ya Maendeleo," amesisitiza Maheda.
Mafunzo hayo yanasimamiwa na kutolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Makao Makuu kwa kuwashirisha wenyeviti na Mameneja, warajisi wasaidizi, na Maafisa Ushirika kutoka Mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Shinyanga pamoja na Mara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.