RC MAKALLA AAGIZA UANDALIWE MPANGO MKAKATI WA KUKUZA SEKTA YA UTALII MKOA WA MWANZA.
*Amuagiza Katibu tawala Mkoa kuandaa kikosi kazi cha kuandaa mpango huo ukihusisha wadau wa utalii
*Awataka kutumia miundombinu inayojengwa kuboresha utalii Mkoani humo*
*Abainisha kuwa mwezi Disemba mkataba wa Ujenzi wa Jengo la abiria uwanja wa Ndege Mwanza utasainiwa*
*Asema Mwanza ina mazingira mazuri ya Utalii wa Ziwa na ipo jirani na Hifadhi za Taifa kama Serengeti*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wadau wa utalii Mkoani humo kutumia fursa ya uwepo wa mazingira rafiki ya ukanda wa ziwa, ujirani na hifadhi za Taifa na uwepo wa vivutio vya utalii kuboresha sekta hiyo kwa kuwekeza kwenye utalii kwa manufaa ya Taifa.
CPA Makalla amesema hayo mapema leo Novemba 30, 2023 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wa kikao kazi na wadau wa utalii kilichokutuna mahsusi ili kujadili na kuweka mpango mkakati wa kuboresha sekta hiyo kwa kutumia mazingira rafiki kwenye ukanda huo uliobarikiwa.
Katika kuhakikisha suala hilo Mkuu wa Mkoa amemuagiza Katibu Tawala Mkoa kuunda kikosi kazi cha kuandaa mpango mkakati huo kikihusisha wataalam kutoka makundi mbalimbali ili kutoka na andiko linalojibu kila swali linalohusu namna gani sekta ya utalii mkoani humo itaboreshwa kwa manufaa ya wana Mwanza na Taifa kwa ujumla.
Amesema uwepo wa ziwa la kihistoria la Victoria, kufikika kwake kwa urahisi na hifadhi za Taifa kama Saanane, Burigi Chato, Rubondo, Rumanyika-Kagera na Serengeti pamoja na uwepo wa vivutio vya kitalii vya kihistoria kama Jiwe linalocheza lililopo Kisiwani Ukerewe, Jengo la Kijerumani la Gunsert na Bujora kunapaswa kusaidia kukuza sekta hiyo.
"Kwa takwimu zilizopo za idadi ya watu kuwa ni Mkoa wa pili, uwepo wa mifugo mingi, uvuvi, kilimo na uwanja wa ndege wa Mwanza ambao unaboreshwa ni ishara tosha kuwa wadau wakijipanga na kuchangamkia fursa zilizopo uchangiaji wa pato la Taifa utapanda na Mwanza itaongoza", amesisitiza.
Katika kuboresha utalii, Makalla amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama ujenzi wa daraja kubwa la Kigongo-Busisi, Meli ya MV Mwanza pamoja na Bandari, Reli ya kisasa na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza pamoja na ujenzi wa jengo la abiria la kisasa ambapo mwezi Disemba mkataba wa ujenzi utasainiwa.
Halikadhalika, Makalla amewataka wataalam hususani kwenye Halmashauri kuweka nia ya kuboresha utalii, kuanisha vivutio vilivyopo na miundombinu inayotakiwa kama mahoteli yenye hadhi na kujipanga na mikakati ya kutenga maeneo yenye hadhi kuendana na utalii ili kujihakikishia kukuza sekta hiyo na kumuunga mkono Rais Samia ambaye amejipambanua kuitegemea sekta hiyo.
"Ndugu viongozi ni lazima tuthubutu kushawishi watu wenye mahoteli na kampuni za kusafirisha watalii, sekta binafsi lazima ihamasishwe, vyuo vikuu na vya kati lazima vichangie kwenye kuwajengea uwezo rasilimali watu na kuhakikisha wanachangia ukuaji wa sekta ya utalii." Mkuu wa Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.