RC MAKALLA AKIPONGEZA CHUO CHA USIMAMIZI WA FEDHA KUJENGA CHUO CHAKE MWANZA
*Aahidi uwepo wa maji ya kutosha kwenye eneo lake la ujenzi baada ya Mradi Mkubwa wa maji kukamilika*
*Akitaka chuo kuipa kipaumbele Mwanza kutokana na kukua kiuchumi*
*Wahitimu watakiwa kuwa wabunifu kupitia taaluma yao kujiajiri wenyewe*
*Atangaza fursa za kiuchumi Mwanza mara baada ya miradi ya kimkakati kumalizika*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla amekipongeza Chuo cha usimamizi wa fedha IFM kwa hatua ya kujenga chuo chake na kuahidi changamoto ya maji eneo la ujenzi itamalizika hivi karibuni kutokana na mradi wa maji Butimba kukamilika.
Akizungumza leo na wahitimu wa ngazi mbalimbali katika mahafali ya 49 ya Chuo cha usimamizi wa fedha IFM kampasi ya Mwanza na Simiyu yaliyofanyika ukumbi wa Rock City Mall, Mkuu huyo wa Mkoa amesema chuo hicho kuwa na majengo yake sasa itakuwa na wigo mpana wa kuwachukua wanafunzi wengi na hasa mahitaji makubwa ya wataalamu wanaohitajika Mkoani humo.
"Ndugu Mwenyekiti wa Baraza la uongozi Prof. Emmanuel Mjema, Mkoa wa Mwanza una miradi mingi ya kimkakati na unachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa,hivyo wataalamu bora kwa upande wa fedha na uchumi watahitajika kutoka Chuoni kwako," CPA Makalla.
Aidha, amewataka wahitimu hao kwenda mtaani kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na siyo vyeti hivyo kwenda kuvifungia kabatini.
"Ni lazima tutambue mara baada ya kutoka hapa suala la ajira bado ni changamoto, hivyo miende mkawe wabunifu wa kujiajiri wenyewe na hasa fursa nyingi za kiuchumi zilizopo Mkoani Mwanza kuanzia Utalii na uchumi wa bluu,"amefafanua Mkuu huyo wa Mkoa wakati anazungumza na wahitimu hao.
CPA Makalla amesema Mkoa wa Mwanza umejaliwa miradi mingi ya kimkakati kuanzia mradi wa reli ya kisasa SGR, Daraja la JP Magufuli,u uenzi wa Meli ya Mv Mwanza pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa, miradi yote hiyo itakapo kamilika itahitaji wataalamu na pia fursa za kujiajiri zitakuwepo kwa wingi.
"Ndugu mgeni rasmi Chuo chetu cha IFM kimezidi kupiga hatua na sasa tuna jumla ya kampasi tatu Mwanza,Dodoma na Simiyu na sasa tupo mbioni kufungua kampasi ya nne huko Mkoani Geita,lengo ni kutoa wataalamu bora hapa nchini," Prof.Emmanuel Mjema,M/kiti wa Baraza la uongozi chuo cha usimamizi wa fedha IFM
Akizungumzia maendeleo ya Chuo hicho Mkuu wa chuo cha IFM Prof. Josephat Mtoto amebainisha walianza na wanafunzi 72 mwaka 1992 na sasa wamepiga hatua kwani mwaka 2022-23 wamekuwa na jumla ya wanafunzi 15,000.
Jumla ya wahitimu 564 wamehitimu masomo yao ya ngazi mbalimbali kuanzia astashahada,shahada na shahada ya uzamili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.