RC MAKALLA ATOA MAAGIZO KUTHIBITI UGONJWA WA KIPINDUPINDU MWANZA
*Awataka wataalam wa afya kila wilaya kuwa na mkakati wa kuhudumia wagonjwa*
*Awataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kutoa elimu ya msukumo wa kila kaya kuwa na choo*
*Aagiza kuwekwa maji tiririka ya kunawa mikono kwenye maeneo yenye mikusanyiko*
*Aagiza taasisi za Serikali na dini kushirikiana kutoa elimu kuhamasisha usafi kwa jamii*
*Asema hakuna gharama kwa mgonjwa wa Kipindupindu kutibiwa, ni bure*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wataalam wa afya kila wilaya kuwa na mikakati ya kudhibiti na kuhudumia wagonjwa wa Kipindupindu kufuatia kuwepo kwa wagonjwa 28 wa Ugonjwa wa Kipindupindu Mkoani humo.
Makalla ametoa wito huo leo Januari 10, 2024 wakati wa kikao chake na wajumbe wa kamati ya huduma ya afya ya msingi Mkoani humo kilichoketi mahsusi ili kuwekeana mikakati ya kudhibiti kusambaa kwa Ugonjwa huo ulioanzia wilayani Magu.
"Tuelewane wataalam wa afya, kama leo tuna wagonjwa 28, tukitoka hapa nataka tudhibiti ugonjwa huu usienee mkoani hapa na ili kufanikisha hilo ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja ya makusudi ya kudhibiti tatizo hili lisisambae tena kwa ushirikiano mkubwa", CPA Makalla.
Aidha, Makalla amebainisha kuwa Kipindupindu kinatokana na vimelea vya uchafu vitokanavyo na matendo kama chakula kuandaliwa bila kunawa mikono na kupelekea mtu kula uchafu na kama mtaani watu wataendelea kuwa na utamaduni wa mama ntilie kuuza chakula kwenye mazingira yasiyo masafi na kwamba mazingira hayo yatafanya ugonjwa kuendelea kusambaa.
"Nataka miwaambie wananchi kwamba hakuna gharama zozote kwa mgonjwa wa kipindupindu kutibiwa, mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Kipindupindu afikishwe hospitalini haraka na sio kumhudumia nyumbani au kwa waganga wa kienyeji na Serikali tumejipanga kuwahudumia." Amesisitiza Makalla.
Vilevile, ameziagiza Mamlaka zote za maji Mkoani humo kuhakikisha maji ni safi na salama kwani yasipotibiwa vizuri yanakua ni sawa na yaliyotoka kwenye mito au malambo na mamlaka za barabara amezitaka zizibueni mifereji ya maji ili yasituame.
"Mapambano haya tutakwenda kushinda kwa muda mfupi kutokana na juhudi ambazo mkoa wameanza kutoa hususani tiba kwa waathirika na ninatoa wito kwa jamii kupeleka wagonjwa hospitali mara moja na taasisi za dini tushirikiane kwa dhati." Mwakilishi kutoka wizara ya sfya.
Mganga Mkuu wa Mkoa Thomas Rutachunzibwa amebainisha kuwa mpaka sasa wilaya zilizoathirika ni tatu za Magu, Nyamagana na Ilemela huku Magu ikiathirika zaidi kwa kuwa na wagonjwa 21 hadi sasa na kwamba tayari kuna vituo vitatu vya kutolea huduma.
"Dalili za kipindupindu zinaanza kujitokeza ndani ya masaa 24 hadi 72 baada ya kupata maambukizi na mtu hukosa maji mwilini kutokana na kutapika na kuharisha hivyo jamii lazima iwe na matumizi sahihi ya vyoo, kuosha chakula kama matunda kwa maji ya moto, kutumia maji yaliyochemshwa na kuchunjwa vizuri." Dkt. Rutachunzibwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.