RC MAKALLA AWATAKA MADIWANI KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO
*Ataka ajenda ya kuthibiti uhalifu iwe ya kudumu*
*Asisitiza nidhamu kazini pamoja na kushirikiana*
*Awataka Misungwi kuitunza miradi ya kimkakati*
*Awataka wazazi kupeleka watoto shule*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Juni 03, 2023 amefika wilayani Misungwi akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha rasmi kufuatia kuhamishiwa kwake Mkoani humo mwishoni mwa mwezi Mei.
Akizungumza na viongozi, watendaji na makundi mbalimbali katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mhe. Makalla amewataka waheshimiwa Madiwani kusimamia miradi ya Maendeleo kwa dhati ili fedha zinazowekezwa huko zioneshe tija kwa kukamilisha miradi yenye ubora na thamani halisi ya fedha.
"Nataka kuwakumbusha juu ya kusimamia kwa dhati miradi ya Maendeleo ili inapokamilika iwe na ubora ila nawapongeza sana kwa kupeleka fedha za miradi ya Maendeleo kwa aslimia 40 na kwenye hili natoa wito kwa waheshimiwa madiwani kutimiza wajibu wao kupitia kamati zao ni lazima wawe na ratiba ya kutembelea na kuikagua miradi." CPA Makalla.
Aidha, Mhe. Makalla ametoa rai kwa viongozi na watumishi wilayani humo kuhakikisha wanakuwa na nidhamu na kuwajibika ipasavyo na kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwa na lugha ya staha na kutoa matumaini kwa jamii.
"Misungwi inakwenda kuwa na kituo cha mizigo kupitia mradi wa reli ya kisasa (SGR) hivyo basi hapa ni sehemu ya kibiashara na mna bahati sana kwani Miradi mikubwa ya kimkakati inagusa wilaya yenu hivyo niwaombe muitunze miradi hii kusiwe na wizi wa vifaa." Mkuu wa Mkoa.
Akitoa taarifa ya Wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Paulo Chacha amesema wilaya hiyo yenye zaidi ya watu laki nne wananchi wake wamekuwa wakijishughulisha na shuguli mbalimbali za kujikwamua kiuchumi zikiwemo Kilimo na Uvuvi kwa zaidi ya asilimia 90 pamoja na biashara na uchimbaji wa Madini.
Aidha, amebainisha kuwa wananchi wa Wilaya hiyo wamenufaika na fidia ya zaidi ya Shilingi Bilioni 7 walizolipwa kupisha maeneo yao kwa utekelezaji wa miradi ya Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na Bandari kavu na wamekuwa wazalendo kuhakikisha uwekezaji wa aina yoyote haukwami.
"Katika kuhakikisha wananchi wa Misungwi wanakuwa na afya njema, afua mbalimbali zinatekelezwa ikiwemo utoaji wa Elimu ya Lishe kwenye shule za Msingi na Sekondari na Ugawaji wa dawa kama za floriki na utoaji wa chakula chenye lishe bora ili kuwakinga watoto na Utapiamlo na kwamba wananchi wanapata huduma ya Maji safi na salama kupitia mamlaka husika." Amefafanua.
Mhe. Chacha anajivunia hati Safi wanazopata mfululizo na amefafanua kuwa Halmashauri hiyo imekua ikikuwa kimakusanyo kila mwaka kutoka Bilioni 2 zilizokusanywa mwaka 2021/22 na Bilioni 3 zilizokusanywa kwenye mwaka 2022/23 na kwamba kwa mwaka 2023/24 wamekadiria kukusanya Bilioni 4.86 na tayari kuna mikakati madhubuti ya kufanikisha hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.