RC MAKALLA AWATAKA PAMBA JIJI FC KUJITUMA NA KUPATA MATOKEO MAZURI UWANJANI
*Asema hafurahishwi na mwenendo wa sasa wachezaji kutokujituma na kupata matokeo yasiyoridhisha*
*Awataka kubadilika kuanzia mchezo wao ujao*
*Awahaidi changamoto zao kuzifanyia kazi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wachezaji wa Pamba Jiji FC kujitafakari haraka kabla ya mchezo wao ujao wa Ligi ya Championship kutokana na matokeo yasiyoridhisha.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ni mlezi wa timu hiyo amezungumza leo Oktoba 10, 2023 mara baada ya mazoezi yao kwenye uwanja wa Nyamagana, amebainisha hali halisi ni wachezaji kutojituma uwanjani ndiyo maana timu imepata matokeo yasiyoridhisha na kushika nafasi ya saba na pointi 7.
"Nimezungumza na makocha kadhaa wa Ligi ya Championship wanasema wazi kabisa tumefanya usajili bora hadi dawati la ufundi lakini changamoto tuliyonayo ni kucheza chini ya kiwango na tusipo badilika haraka itatugharimu", CPA Makalla.
Ameongeza kuwa lengo ni timu kucheza Ligi kuu msimu ujao ndiyo maana imefanyiwa maandalizi mazuri ya kutoka kuchangiwa bakuli na sasa inamilikiwa na Halmashauri ya Jiji na endapo hakutakuwa na mabadiliko juhudi za haraka za kuongeza nguvu za wachezaji kutoka nchi jirani zitafanywa wakati wa dirisha dogo.
CPA Makalla akiwa ameambatana na baadhi ya wachezaji wa zamani wa Pamba FC akiwemo Fumo Felician naye alipata wasaa wa kuwatia shime kucheza kwa bidii kama walivyofanya wao miaka ya nyuma.
"Tambueni mnaichezea timu yenye jina kubwa hapa nchini,huu ni wakati wa kutupa matokeo mazuri kutokana na mazingira mliyonayo,sisi miaka ya nyuma maslahi hayakuwa makubwa zaidi ya kucheza kwa uzalendo na kuupambania Mkoa". Fumo Felician, mshambuliaji wa zamani,Pamba FC
"Mhe.Mkuu wa Mkoa tumekusikia ila changamoto inayotukabili ni timu nyingi kutupania kila tukicheza nazo, tunatambua matokeo haya hayawafurahishi mashabiki wa soka tunawaahidi kujirekebishia,"Jerry Tegete,Nahodha wa timu.
Pamba Jiji FC baada ya kucheza michezo 5 ikishinda miwili, imepoteza mmoja na kutoka sare, hata hivyo jumamosi hii itashuka uwanja wa nyumbani Nyamagana kupepetana na Green Warriors.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.