RC MAKALLA AWATAKA VETA KUWA NA KOZI RAFIKI KWA MAHITAJI YA WANANCHI WA KISIWA CHA UKEREWE
*Amuagiza Afisa Elimu kuwajuza Wakuu wa Shule na Walimu wakuu kuhusu kuanza kwa masomo mwezi januari kwenye chuo hicho*
*Aagiza Baraza la Madiwani kushirikiana na kamati za maendeleo za kata kuhamasisha wananchi kupeleka vijana VETA*
*Amtaka Afisa Habari wa Halmashauri hiyo kupeleka matangazo redioni kuwajulisha wananchi uwepo wa chuo*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ametoa rai kwa uongozi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kuweka kozi fupi na zinazozingatia mahitaji ya eneo husika ili kuleta tija zaidi ya uwepo wa vyuo hivyo nchini kwa kupata vijana wengi zaidi kujifunza na kujiendeleza kwenye shughuli za kiuchumi.
Amesema hayo leo tarehe 23 Novemba, 2023 wakati akikagua ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichogharimu zaidi ya Bilioni 2.6 kwenye kijiji cha Muhula kwenye kisiwa cha Nansio wilayani Ukerewe huku kikitarajiwa kudahili zaidi ya wanafunzi 700 kwa wakati mmoja.
"Niwaombe uongozi wa VETA muwe na kozi zinazolenga mahitaji ya wananchi moja kwa moja, tunataka vijana wetu sasa wawe na ujuzi wa kutengeneza Boti na mbinu za kujihusisha na uvuvi wa kisasa ili watu wetu waweze kujiimarisha na kujiinua kiuchumi." Amesisitiza Makalla.
Aidha, amuagiza Afisa Elimu wa wilaya hiyo kuwajuza Wakuu wa Shule na Walimu wakuu kuhusu kuanza kwa masomo mwezi januari kwenye chuo hicho ili wawajuze wanafunzi wanaohitimu juu ya faida za uwepo wa fursa hiyo ambayo inawapa ujuzi wa vitendo moja kwa moja.
Vilevile, kupitia Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ameliagiza Baraza la Madiwani kushirikiana na kamati za maendeleo za kata ili kuhamasisha wananchi kupeleka vijana kupata elimu ya Stadi za maisha ambapo itasaidia kufikisha elimu kwenye ngazi za chini hususani vitongojini na kwenye vijiji.
Katika kuhakikisha ujumbe wa uwepo wa fursa hiyo unafika kwa wananchi wote wa wilaya hiyo yenye visiwa vidogo 38, Mhe. Makalla amemtaka Afisa Habari wa Halmashauri hiyo kupeleka matangazo kwenye redio hususani za kijamii zinazosikika visiwani humo kuwajulisha wananchi kwani njia hiyo itarahisisha kupeleka taarifa kwa haraka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.