RC MAKALLA AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI UKARA WA ZAIDI YA BILIONI 4.5
*Amshukuru Rais Samia kwa kuwaletea wananchi wa kisiwa hicho maji safi*
*Mradi huo wafikia asilimia 80 ya utekelezaji*
*Aahidi kufuatulia fedha za ukamilishaji wa kradi huo*
*Awasihi wananchi kuutunza mradi kwa manufaa ya muda mrefu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Novemba 22, 2023 ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Ukara unaotekelezwa na Mkandarasi M/S Halem Construction Company Limited kwa zaidi ya shs bilioni 4.5 chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Ukerewe.
Akizungumza na wananchi kwenye chanzo cha mradi huo Mhe. Makalla amemshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha hizo kwa ajili ya kuwapatia maji safi wananchi zaidi ya elfu 40 wa kisiwani humo ambao wataondokana na adha ya kuugua magonjwa ya tumbo na hatari ya kuliwa na Mamba.
Makalla amesema nia ya dhati ya Rais Samia kwa wananchi wake wa vijiji vinane ni lazima itimie na kwenye hilo atahakikisha anafuatilia fedha za mradi huo ili mkandarasi aweze kulipwa na amemtaka kuendelea na kazi na kuhakikisha anakamilisha mradi huo muhimu kwa jamii.
"Niwahakikishie kwamba kazi hapa haita simama, ninakwenda kulifanyia kazi suala la fedha za mradi huu na mkandarasi abaki eneo lake la kazi aendelee kwani atakua shuhuda na wananchi wataona mabadiliko makubwa muda si mrefu." Makalla.
Aidha, ametumia wasaa kuwapongeza wabunifu wa mradi huo kwa kutumia nishati ya jua ambayo itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji na amewasihi wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo ili mradi wao uweze kujiendesha na kuwasaidia kwa muda mrefu.
"Kukamilika kwa mradi huu utakaosaidia wananchi kwenye vijiji 8 ni ishara ya kuondokana na maradhi ya tumbo na Rais Samia amedhamiria kuwafikia wananchi kwenye vijiji vyote 76 kwenye jimbo letu." Amezungumza Mhe. Joseph Mkundi Mbunge wa Ukerewe kwa niaba ya wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ukerewe Mhe. Ally Mambile amemshukuru Rais Samia kwa kuwajali wananchi wa vijiji vya Bwisya, Bukungu, Chifule, Chibasi, Nyang'ombe, Nyamanga, Kome na Bukiko na amebainisha kuwa Ilani ya chama hicho anaitekeleza vema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.