RC MAKALLA AZINDUA BOTI 5 ZA DORIA WILAYANI UKEREWE, KUSAIDIA KUZUIA UVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA
*Kusaidia kuongeza Usimamizi wa Shughuli za Uvuvi na kuzuia Uvuvi haramu*
*Kusaidia kuongeza ukusanyaji wa Mapato ya ndani ya Halmashauri*
*Zitasaidia kurahisisha usafiri na kuboresha shughuli za uokozi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo novemba 23, 2023 amezindua Boti tano zilizokarabatiwa kwa zaidi ya Milioni 400 ambazo zitasaidia kufanya doria na kuongeza usimamizi wa shughuli za ziwani hususani kuthibiti uvuvi haramu.
Akizungumza na wananchi kwenye hafla hiyo Mhe. Makalla ameipongeza Halmashauri ya Ukerewe kwa kuchangia fedha zaidi ya Milioni 100 kwenye mradi huo kutoka kwenye fedha za mapato ya ndani kwani boti hizo ni nyenzo sahihi kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri.
Amesema pamoja na shughuli za doria ziwani, boti hizo zitasaidia kurahisisha usafiri kwenye mwambao wa ziwa victoria na hasa uokozi wakati wa dharula na kwamba wananchi kwa ukusanyaji wa mapato wataboreshewa huduma zingine za kijamii kwenye sekta za Afya, elimu na kwingineko.
"Tuepuke kutumia mabomu na njia zingine haramu za uvuvi ili tulinde ziwa letu na rasilimali zilizomo kama Samaki," amesema Mkuu wa Mkoa wakati akifafanua kuhusu madhara ya Uvuvi haramu.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametumia wasaa huo kuwataka maafisa uvuvi na watendaji kutumia boti hizo kuwafikia wananchi visiwani na kutoa elimu ya kuhakikisha wananchi wanaachana na uvuvi haramu na utoroshaji wa Samaki badala yake wananchi wahamasishwe kufanya uvuvi wa kisasa.
"Lengo tulilojiwekea la kufikia kiwango cha makusanyo kulingana na bajeti yetu litatimia kwa kutumia nyenzo hizi kwa mujibu wa matakwa yake na wala hatutazitumia kwa shughuli za anasa." Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Joshua Manumbu.
Katika wakati mwingine, Mhe. Makalla amekagua ujenzi wa jengo la halmashauri linalotekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 3 na amewataka halmashauri hiyo kuongeza usimamizi ili kumaliza ujenzi kwa wakati ili wananchi wapate huduma kwenye jengo hilo la kisasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.