*RC Malima Awataka Wazazi Kupeleka watoto Shule Sengerema*
Halmashauri ya wilaya ya Sengerema imekamilisha Ujenzi wa vyumba vya Madarasa 152 yenye thamani ya Tshs Bilioni 3.04 kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023 ambapo jumla ya wanafunzi 9451 waliofaulu wanaendelea kuripoti na kusajiriwa kwa ajili ya kuanza mwaka wa masomo.
Hayo yamebainishwa leo Jumamosi Januari 14, 2023 wakati wa hafla ya makabidhiano ya Madarasa hayo yakiwa na samani kwenye shule ya Sekondari Nyampulukano ambapo Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amekagua na kupokea Madarasa Matano kwa niaba ya Wilaya nzima.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amewataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wote waliofaulu kidato cha kwanza haraka iwezekanavyo ili wapate elimu bora ambayo Mhe. Rais amewaletea kwa kuwajengea vyumba nadhifu vya Madarasa vyenye Samani.
"Wazazi na walezi hakikisheni watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wanapelekwa shule kufikia Jumanne (Januari 17, 2023), mzazi atayefika jumatano hajapeleka mtoto shule atachukuliwa hatua kali za kisheria maana namna pekee ya kumshukuru Mhe. Rais ni kuhakikisha watoto wanasoma kupitia madarasa haya mazuri aliyotujengea." Mkuu wa Mkoa.
"Mapato ya ndani ya Halmashauri hii hayazidi Bilioni Mbili lakini Mhe. Rais ametuletea zaidi ya Bilioni tatu kwa ajili ya kujenga vyumba vya Madarasa, hii ina maana kwamba tungesema tujenge kwa kutumia mapato ya ndani tusingefanikiwa hivyo namshkuru na kumpongeza sana Mhe. Rais kwa kuupiga mwingi" Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga.
Katibu Tawala Mkoa, Ndugu Balandya Elikana ametoa shukrani kwa Mhe. Rais kwa kuwezesha wanafunzi wote waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza kwa wakati mmoja kutokana na fedha alizotoa kujenga vyumba vya Madarasa na miundombinu ya kujifunzia kwa ujumla na ametoa wito kwa watoto kuendelea kuripoti shuleni kutumia fursa hiyo adhimu.
Akitoa taarifa ya Ujenzi, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Binuru Shekidele amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo imefanya Halmashauri kuwa na vyumba 215 wakati mahitaji yalikua vyumba 210 hivyo Halmashauri imekua na ziada ya vyumba vya Madarasa Matano na ukamilishaji huo utachochea zaidi kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.