Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Adam Malima leo Agosti 24 ameendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi leo ikiwa ni siku ya pili ametembelea Wilaya ya Sengerema Halmashauri ya Buchosa Kata ya Nyehunge.
Akizungumza na Karani wa Sensa katika moja ya kaya iliyopo Kata ya Nyehunge aitwaye Lucy Lucas Lubala, Mhe. Malima amesema Makarani wa Sensa wanatakiwa kukadiria kaya watakazozihesabu kwa siku ili waruhusu watu waendelee na shughuli zao za kila siku.
" Karani kama jana umehesabu nyumba 25 leo unaweza kukadiria walau kaya 30 ili kaya zitakazobaki bila kufikiwa waalikwe kiubalozi, amesema Mhe.Malima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe.Senyi Ngaga amesema wamejiandaa vizuri kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza ili kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake Thomas Ngusa mshauri wa Kitongoji cha Senta Magharibi - Nyehunge amesema kwa upande wao walijigawa kiubalozi kwa hiyo hawakukaa kitongoji kizima nyumbani ili kusubiri Karani badala yake walipata maelekezo mazuri, wanakwenda ubalozi kwa ubalozi.
Baada ya maelezo ya Ngusa Mhe.Malima aliwapongeza wananchi na viongozi wa Kata ya Nyehunge kwa kuweka utaratibu wa kuwaachia wananchi kuendelea na shughuli zao badala ya kuwaambia wakae nyumbani kwao kusubiri Karani wa Sensa.
Hata hivyo, amewaomba wananchi wa Nyehunge kuendelea kutekeleza kikamilifu na kukumbushana kuhusu umuhimu wa kuhesabiwa kwani zoezi lilianza jana tarehe 23.8.2022 na linaendelea Nchi nzima kwa siku saba
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.